Hatimaye Adebayor yupo Man City!!
Klabu ya Manchester City imekamilisha uhamisho wa Mchezaji kutoka Togo Emmanuel Adebayor, miaka 25, kwa Pauni Milioni 25 baada ya kuichezea Arsenal kwa miaka mitatu na nusu akitokea Monaco ya Ufaransa.
Adebayor msimu uliokwisha aliifungia Arsenal mabao 16 na kujiunga kwake na Man City kutaimarisha Kikosi hicho ambacho tayari kishawabeba Washambuliaji Carlos Tevez na Roque Santa Cruz na Kiungo Gareth Barry.
Baada ya kukamilika taratibu hizo za uhamisho, Adebayor alitamka: ‘Nimezaliwa kucheza mpira na hilo ndilo nataka kufanya. Nawashkuru Man City kwa mapokezi mazuri!’
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amethibisha uhamisho huo wa Adebayor upo na amedai kupona kwa Mafowadi Thomas Rosicky na Eduardo kutaziba pengo la kuondoka kwa Adebayor.
Wenger amesema: ‘Tutamkosa Adebayor lakini ni bora tu tuangalie Wachezaji tuliokuwa nao. Namtakia kila la kheri na kumshukuru kwa mchango wake Arsenal.’
MECHI ZA KIRAFIKI:
-Seattle Sounders 0 Chelsea 2
Mchezaji mpya wa Chelsea Daniel Sturridge alifunga bao lake la kwanza kwa Klabu yake mpya na kumtengenezea Frank Lampard kufunga la pili na kuwafanya Chelsea washinde mechi yao ya kwanza huko ziarani Marekani mjini Seattle kwa kuifunga Timu ya Seattle Sounders mabao 2-0.
-Barnet 2 Arsenal 2
Arsenal, wakicheza mechi yao ya kwanza ya kirafiki ikiwa ni matayarisho ya msimu mpya, wametoka suluhu na Timu ya Daraja la chini Barnet kwa mabao 2-2 huko mjini London.
Mabao ya Barnet yalifungwa na Yakubu dakika ya 45 na la pili dakika ya 83 na Charles.
Wafungaji wa Arsenal ni Arshavin dakika ya 44 na Barazite dakika ya 49.
-Man U wakubali kurudiana na Malaysia
Manchester United, wakiwa ziarani huko Asia, wamekubali kurudiana na Malaysia mjini Kuala Lumpur siku ya Jumatatu baada ya kuifunga Nchi hiyo mabao 3-2 siku ya Jumamosi.
Jumatatu Manchester United walitakiwa kucheza Jakarta, Indonesia lakini ziara ya huko imefutwa kufuatia kulipuliwa kwa Hoteli ambayo Man U walipangiwa kufikia.
Baada ya mechi hiyo Nchini Malaysia, Man U wataruka hadi Korea ya Kusini kucheza na Klabu ya FC Seoul mjini Seoul, Korea hapo Ijumaa.
No comments:
Post a Comment