Wamiliki wa Man U Familia ya Glazer wadai 'vijisenti' vipo!!!
Wamiliki wa Manchester United, Familia ya kina Glazer, wamesisitiza kuwa Meneja wa Timu yao Sir Alex Ferguson analo bulungutu lililoshiba la kununua Mchezaji anaemtaka ila hawategemei kuwa atatumia ovyo pesa hizo.
Manchester United wamepata Pauni Milioni 80 kwa mauzo ya Cristiano Ronaldo kwa Real Madrid lakini wametumia pesa kidogo tu ambazo hazizidi Pauni Milioni 20 katika kununua wachezaji wapya.
Mpaka sasa Man U imemchukua Michael Owen bila gharama kwa vile alikuwa Mchezaji huru pamoja na Winga Luis Antonio Valencia, Kiungo Gabriel Obertan na Mshambuliaji Mame Biram Diouf.
Msemaji wa Wamiliki hao kina Glazer, Tehsin Neyani, ametamka: ‘Meneja anazo pesa za kununua Wachezaji. Tunazungumzia kiasi cha Pauni Milioni 60.”
Hata hivyo Sir Alex Ferguson mwenyewe ametangaza hasajili tena lakini Msemaji wa kina Glazer, Tehsin Neyani ameendelea kusema: ‘Meneja hajapata Wachezaji wanaofiti falsafa ya Man U. Hatununui Wachezaji mamluki!’
Gerrard amwomba Pilato msamaha!
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, leo akitoa ushahidi wake Mahakamani katika kesi inayomkabili ya kushambulia na kujeruhi, ameiomba Mahakama msamaha ingawa amedai alirusha ngumi kwa kujihami kwani alidhani Marcus McGee angemshambulia.
Gerrard alisema: ‘Ni kweli nimekosea kwani nilifikiri atanishambulia.”
Gerrard alidai alipewa ruhusa na Meneja wa Naitiklabu waliyokuwepo kuchagua muziki na alipokuwa akiangalia kadi ya muziki McGee akaja na kuipora mkononi kwake na wakaanza kubishana kisha yeye Gerrard akaondoka lakini akarudi tena dakika chache baadae.
Gerrard alisema aliwaambia Polisi kuwa alidhani McGee atamshambulia kwani alimsogolea lakini hakujua kusogea kwa McGee ni kwa sababu alikuwa amepigwa na wenzake Gerrard.
Kesi inaendelea.
Southgate anategemea Mido na Tuncay kuondoka Boro
Meneja wa Middlesbrough Gareth Southgate anategemea Wachezaji wake Mido na Tuncay Sanli kuondoka klabuni hapo katika wiki chache zijazo.
Southgate alisema: "Tunajua Mido na Tuncay hawataki kukaa Timu ya Daraja la chini na nina uhakika wanunuzi watakuja.’
Middlesbrough iliporomoka Daraja kutoka Ligi Kuu England msimu uliokwisha na msimu ujao watacheza Coca Cola Championship.
No comments:
Post a Comment