Saturday 1 August 2009

KOMBE LA EMIRATES: Kuanza leo Nyumbani kwa Arsenal!
Leo jioni, Timu za Arsenal, Glasgow Rangers kutoka Scotland, Paris Saint-Germain [PSG] kutoka Ufaransa na Atletico de Madrid ya Spain zitashuka Uwanja wa Emirates kugombea Kombe la Emirates ikiwa ni maandalizi ya Timu hizo kwa msimu mpya utakaoanza hivi karibuni.
RATIBA: [saa za bongo]
Jumamosi, Agosti 1
Saa 10 jioni: Rangers v PSG
Saa 12 na dak 15 jioni: Arsenal v Attletico
Jumapili, Agosti 2:
Saa 10 jioni: Atletico v PSG
Saa 12 na dak 15 jioni: Arsenal v Rangers
Wolfsburg wakamilisha uhamisho wa Martins!
Mabingwa wa Ujerumani Wolfsburg wametangaza rasmi kuwa Obafemi Martins amesaini mkataba wa miaka minne kwa dau la Pauni Milioni 9.
Martins, anaetoka Nigeria, amekuwa akicheza Newcastle Timu iliyoporomoka Daraja kutoka Ligi Kuu England, tangu atoke Inter Milan mwaka 2006.
Ferguson kubadili mbinu Man U
Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amekiri kuwa inabidi abadilishe mbinu za uchezaji baada ya Mfungaji wao mkuu kwa misimu miwili iliyopita Cristiano Ronaldo kuondoka.
Ferguson amekiri: “Ni pigo kuu Cristiano kuondoka. Inabidi tutafute magoli kwa njia nyingine. Mbinu zitabadilika.”
Msimu uliokwisha Ronaldo alifunga goli 26, Berbatov 14 na Rooney 13.
Ferguson aliongeza: “Huko nyuma, Scholes, Giggs na Beckham kila mmoja alikuwa akifunga mabao 10. Lakini siki hizi magoli toka kwa Viungo wetu yamekauka. Inabidi tushughulike hilo. Pia itabidi kina Park, Nani, Valencia, Welbeck na Macheda wafunge jumla ya goli 40 kati yao!"
Mutu ashindwa rufaa kupinga kulipa Mamilioni!
Adrian Mutu inabidi ailipe Chelsea Pauni Milioni 4.65 baada ya kushindwa rufaa yake iliyopinga uamuzi wa FIFA wa kumtaka alipe kiasi hicho kwa Chelsea ikiwa ni fidia ya kukiuka mkataba.
Mshambuliaji huyo kutoka Rumania alieigharimu Chelsea Pauni Milioni 15 mwaka 2003 alifukuzwa Chelsea mwaka mmoja baadae baada ya kugundulika anatumia cocaine na kufungiwa miezi 7 kutocheza soka.
FIFA iliamua Mutu ailipe Chelsea pesa hizo zikiwa ni fidia lakini Mutu alikata rufaa kupinga uamuzi huo kwa Korti ya Masuala ya Michezo [CAS= Court of Arbitration for Sport].

Baada ya kutimuliwa Chelsea, Mutu alijiunga na Juventus Januari 2005 na msimu mmoja baadae akaenda Fiorentina ambako yuko mpaka leo.

No comments:

Powered By Blogger