Monday 31 August 2009

Terry asaini mkataba mpya Chelsea
Nahodha wa Chelsea John Terry amesaini mkataba mpya wa miaka mitano na Klabu yake Chelsea na inasemekana atakuwa akilipwa mshahara wa Pauni 150,000 kwa wiki.
Mlinzi huyo alikuwa akiandamwa na Manchester City lakini Chelsea waligoma kumuuza Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ambae pia ni Nahodha wa England.
Terry amekuwa yupo na Klabu ya Chelsea tangu akiwa na miaka 14 na ameshashinda Ligi Kuu mara 2, FA Cup mara 4, Kombe la Ligi mara 3 pamoja na Kombe la Ulaya zamani likiitwa Kombe la Washindi.
Terry amechezea Chelsea mara 276 na kufunga goli 17 na pia ameichezea England mara 54 tokea mwaka 2003.
Wolves wamnasa Castillo toka Ecuador
Wolverhamton, moja ya Timu 3 zilizopanda Daraja msimu huu na sasa ipo Ligi Kuu England, imemsaini Kiungo kutoka Nchi ya Ecuador Segundo Castillo kwa mkopo kutoka Klabu ya Serbia Red Star Belgrade.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 tayari yupo kambini na wenzake baada ya kufaulu upimaji afya.

Msimu uliopita Castillo alichezea mechi 13 Everton alikokuwa kwa mkopo.
Huyu ni Mchezaji wa pili kwa Wolves kumsaini kutoka Red Star Belgrade baada ya kumchukua Nenad Milijas mwezi Juni na anakuwa Mchezaji wa 8 kusainiwa na Wolves kwa ajili ya msimu huu wengine wakiwa pamoja na Milijas, Marcus Hahnemann, Kevin Doyle, Andrew Surman, Greg Halford, Ronald Zubar na Michael Mancienne.
Baada ya kutandikwa na Man U Wenger azidi kunung’unika!
Arsene Wenger wa Arsenal ameendelea kunung’unika safari hii akiisakama Manchester United ambao waliifunga timu yake Arsenal bao 2-1 hapo Jumamosi kwenye mechi ya Ligi kuu kwa kudai Man U walitumia mbinu ambazo ni kinyume na Soka na kucheza rafu ili kuidhibiti timu yake.
Wiki iliyopita Wenger aliishambulia UEFA mara baada ya Chama hicho cha Soka Ulaya kumfungulia mashtaka Mchezaji wake Eduardo kwa kumdanganya Refa pale alipojidondosha ndani ya boksi na kujifanya Kipa wa Celtic ndie aliemwangusha na hivyo kupata penalti aliyoifungia Arsenal bao la kwanza katika ushindi wa 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa nyumbani kwa Manchester United, Old Trafford, Arsenal ndio Timu iliyopewa Kadi nyingi na Refa Mike Dean aliyewapa Wachezaji wa Arsenal Kadi za Njano 6 na hivyo kuifanya Arsenal ilimwe faini ya Pauni 25,000 na pia Wenger mwenyewe alitolewa nje ya uwanja pale alipopiga teke chupa ya maji kwenye dakika za majeruhi.
Hata hivyo Wenger anadai Wachezaji wa Man U walikuwa wakicheza rafu na hawakuwa wakipewa Kadi na hilo analiona ni kosa kubwa kupita ile tabia ya Wachezaji wake kujidondosha.
Katika mechi hiyo Mchezaji wake Eboue alijidondosha makusudi bila kuguswa akiwa na dhamira ya Evra wa Man U apewe Kadi lakini Refa alikuwa makini na kumgundua na kumtwanga Kadi ya njano.
Manchester United hawajajibu chochote mpaka sasa kuhusu shutuma za Wenger.

No comments:

Powered By Blogger