Saturday, 5 September 2009

KIVUMBI LEO: Argentina V Brazil!!!
Brazil wabeba maji ya kunywa kwenda nayo Argentina!!!
Timu ya Taifa ya Brazil imefungasha hadi maji yao ya kunywa kwa safari ya kwenda Argentina kupambana na wenyeji wao Argentina katika mechi muhimu sana ya mtoano ya Kombe la Dunia itakayochezwa leo saa 6 na nusu usiku [bongo taimu] Rosario City, Argentina.
Mechi hii ni muhimu sana kwa Argentina hasa kwa vile wako nafasi ya 4 na pointi 5 nyuma ya Brazil wanaoongoza Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini ambalo litatoa Timu 4 kuingia Fainali na ya 5 itachuana na Timu moja toka Kundi la Nchi za Marekani ya Kati, Kaskazini na Nchi za Caribean.
Nyuma ya Argentina kwa pointi 2, kwenye nafasi ya 5, yuko Ecuador.
Brazil wakishinda mechi ya leo na mechi nyingine kwenye Kundi hili yakienda upande wa Brazil basi Brazil atafuzu kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani.

Pengine Brazil wamekumbuka kauli ya Diego Maradona, ambae sasa ndie Kocha wa Argentina, aliyoitoa kwenye TV za Argentina kwamba kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990 huko Italia, Argentina walinyunyiza dawa za usingizi kwenye chupa ya maji ya Brazil. Argentina walishinda mechi hiyo 1-0 na kuwatoa mashindanoni Brazil.
AFA, Chama cha Soka cha Argentina, kilipinga kauli hiyo ya Maradona lakini mpaka leo Brazil wanaamini maneno ya Maradona.
Hata hivyo, Rodrigo Paiva, Afisa Habari wa Brazil, amepinga Brazil wanaogopa kudhuriwa na alisema hiyo ni tahadhari ya kawaida tu wanayoifanya kila wanaposafiri nje.
Uhasimu kati ya Nchi mbili hizi za Marekani ya Kusini ni wa siku nyingi sana na mkubwa sana kiasi ambacho wengi wanaamini chochote kinaweza kutokea.
DWIGHT YORKE ASTAAFU!!!!
Dwight Yorke, Fowadi wa zamani wa Manchester United, amestaafu kucheza Soka baada ya kuachwa na Timu yake ya mwisho Sunderland mwishoni mwa msimu uliopita.
Yorke, 37, alishinda Kombe la UEFA CHAMPIONS LEAGUE mwaka 1999 na Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 3 mfululizo akiwa na Manchester United kwa kipindi cha miaka minne. Vilevile aliiongoza Nchi yake Trinidad and Tobago kama Nahodha kwenye Kombe la Dunia mwaka 2006.
Yorke amekubali kuwa Meneja Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Trinidad and Tobago ikiwa ni hatua ya kwanza ya kujiingiza kuwa Kocha wa Timu.
Yorke ametamka: “Ni wakati wa kustaafu. Bado nipo hali nzuri lakini umri unakwenda. Nadhani watu watasema nilicheza inavyostahili siku zote nikiwa na furaha usoni mwangu.”
Yorke aliongeza: “Nimebarikiwa sana! Nimecheza pamoja na Wachezaji bora duniani ambao hawajapata kutokea kwenye Ligi kuu akina Roy Keane, Paul Scholes, Ryan Giggs, David Beckham, Peter Schmeichel na chini ya Meneja Bora kuliko wote Sir Alex Ferguson!!”
Yorke akamalizia: “Siku zote nitajiona nina bahati! Nilikuwa ni mtoto kutoka bichi ya Kisiwa kidogo cha Caribean aliepata bahati kubwa ya kutimiza ndoto yake ya kushinda Vikombe!!”

No comments:

Powered By Blogger