Friday, 4 September 2009

KOMBE LA DUNIA: Argentina v Brazil
Maradona: Lazima tushambulie!!
Jumamosi, Argentina wanawakaribisha mahasimu wao Brazil kwenye kinyang’anyiro cha mtoano kuwania kuingia Fainali Kombe la Dunia kwa Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini huku Brazil akiwa ndie kinara wa Kundi hilo akiwa pointi moja mbele ya Chile na pointi 5 mbele ya Argentina walio nafasi ya 4 wakifukuzwa na Ecuador walio nafasi ya 5 na pointi 2 nyuma ya Argentina.
Timu 4 za juu za Kundi hili zitaingia moja kwa moja Fainali huko Afrika Kusini na Timu ya 5 itacheza mchujo na Nchi kutoka Kundi la Marekani ya Kati, Kaskazini na Nchi za Carribean.
Akitambua umuhimu wa kufanya vizuri kwenye mechi hii ya Mahasimu hao, Kocha wa Argentina, Diego Maradona, aliomba mechi hii ihamishwe kutoka Buenos Aires hadi Rosario City ambako, ingawa Kiwanja ni kidogo, lakini mashabiki wa huko wanahamasisha sana Nchi yao.
Maradona amewataka wachezaji wake kushambulia muda wote na kutowapa Brazil nafasi ya kupumua.
Maradona amejigamba: “Tutashambulia kupitia wingi tukiwatumia Maxi Rodriguez na Jesus Datolo, katikati kupitia Juan Sebastian Veron huku Messi na Tevez wakileta kizaazaa na Javier Zanetti akipanda toka nyuma!”
Endapo Brazil ataifunga Argentina na matokeo ya mechi nyingine yakaangukia kwao Brazil, basi Brazil watatinga Fainali huku Kundi hili likibakiwa na mechi 4 kwa kila Nchi.
Staa wa Brazil, Robinho, alipohojiwa alitamka: "Watatumia mabavu kama kawaida yao! Na sisi tutacheza kwa nguvu lakini tutaucheza mpira! Wao wanataka kuifanya mechi hii kama vita lakini sisi tutacheza soka na kufunga magoli.”

No comments:

Powered By Blogger