Friday 4 September 2009

CHELSEA KUKATA RUFAA
Baada ya kufungiwa na FIFA kutofanya usajili wa Mchezaji yeyote kwa vipindi viwili vya usajili, yaani kile cha Januari, 2010 na kile cha Mei hadi Agosti, 2010, ikimaanisha wataruhusiwa kufanya usajili Januari, 2011, Chelsea imesema itakata rufaa kupinga uamuzi huo.
Adhabu ya Chelsea imetokana na kupatikana na hatia ya kumrubuni na kumsajili Kijana Gael Kakuta, miaka 18, kinyume cha taratibu mwaka 2007 kutoka Klabu ya FC Lenz ya Ufaransa ambayo ilipeleka malalamiko yake FIFA.
Mwezi Aprili mwaka huu, FIFA iliipa Klabu ya Uswisi FC Sion adhabu kwa kosa kama la Chelsea na ikaamriwa kutosajili hadi 2010 kwa kumsaini Kipa wa Misri, Essam El Hadary, aliekuwa Klabu ya Al-Ahly, kinyume cha kanuni.
Kama Gael Kakuta, Kipa El Hadary alifungiwa miezi minne.
Lakini FC Sion wakakata Rufaa Mahakama ya Rufaa ya Michezo [CAS=Court of Arbitration of Sports] na, huku kesi ikiiendelea na uamuzi unasemekana utatoka baadae mwaka huu, FC Sion iliruhusiwa kufanya usajili kama kawaida.
Mwaka 2005, Chelsea ilipigwa faini na Ligi Kuu England baada ya kugundulika wao na Kocha wao wakati huo, Jose Mourinho, walimrubuni kinyume cha sheria, aliekuwa Beki wa Arsenal wakati huo, Ashley Cole.
MAN U KUYAKUTA YA CHELSEA?
Wakati Chelsea wanaweweseka na pigo toka FIFA la kufungiwa hadi 2011 kufanya usajili, Klabu nyingine ya Ufaransa, Le Havre inayocheza Daraja la Chini Ligi 2, imedai Manchester United imemrubuni na kumsajili Chipukizi wao aitwae Pogba, miaka 16, kinyume cha taratibu na wako mbioni kuwashtaki FIFA.
Machester United imekanusha madai hayo na, hata hivyo, usajili wa Chipukizi huyo kwenda Manchester United haujakamilika.
Msemaji wa Manchester United amesisitiza: “Ni upumbavu mtupu! Sisi siku zote tunafuata kanuni za UEFA."
Lakini, Mkurugenzi Mtendaji wa Le Havre Alain Belsoeur anapinga na kudai wao wanao ushahidi wa kimaandishi kuwa Man U walitoa vivutio kwa Pogba.
Alain Belsoeur amedai: “Tunaendelea na kesi yetu. Tuna uhakika tutashinda si kwa manufaa ya Klabu tu bali dunia yote ya Soka!”

No comments:

Powered By Blogger