Saturday, 5 September 2009

SAKATA LA CHELSEA KUSAINI “MTOTO”!!!! Klabu nyingine Ufaransa yatishia kuishitaki Chelsea FIFA!! Baada ya FC Lenz kuishitaki Chelsea FIFA kuhusu Kijana Gael Kakuta na kufanikiwa kuisulubisha Klabu hiyo ya London adhabu ya kutosajili hadi 2011, Klabu nyingine ya Ufaransa, ASPTT Marseille, ambayo si Klabu ya Soka ya Kulipwa, imetishia kwenda FIFA kuhusu Mtoto wa miaka 11, Jeremy Boga, aliechukuliwa na Chelsea Oktoba mwaka jana.
ASPTT Marseille inadai Chelsea wamefanikiwa kumchukua Boga baada ya kuwapatia nyumba na gari Wazazi wa mtoto huyo jijini London jirani na Stamford Bridge.
Chelsea wamesema hawakuvunja sheria yeyote kwa vile Mtoto huyo ni chini ya miaka 12 na hivyo hamna sheria inayotaka kupata Cheti cha Uhamisho wa Kimataifa kwa mtoto wa umri huo.
Chelsea yapata matumaini kidogo toka CAS, Mahakama ya Usuluhishi Michezoni!!!!
Huenda Chelsea wakaruhusiwa kusaini Wachezaji wapya wakati Dirisha la Uhamisho likifunguliwa tena Januari 2010 mbali ya kuwa kifungoni hadi 2011 kutosajili Mchezaji kwa kukiuka sheria za usajili walipomchukua Chipukizi Gael Kakuta toka FC Lenz.
Matumaini hayo yamekuja baada ya ufafanuzi kutoka CAS [Mahakama ya Usuluhishi Michezoni] kwamba endapo Chelsea watachelewesha kukata rufaa kwao na kuutumia muda wote wa kuwasilisha rufaa ndani ya siku 21, Mahakama hiyo itabidi icheleweshe kusikilizwa kesi hiyo na pia kuchelewa kutolewa uamuzi.
Kawaida wakati Timu inapokata rufaa kwa CAS adhabu yao husimamishwa hadi uamuzi utolewe.
Katibu Mkuu wa CAS, Mathieu Reeb, ametoa ufafanuzi: “Inategemea lini Chelsea wanakata Rufaa. Wakikata Rufaa wiki hii au ijayo, basi sisi tutapanga kusikiliza kesi Novemba na Desemba uamuzi utatoka. Lakini wakichelewesha na kutumia karibu siku zote 21 za kukata rufaa baada ya kupewa adhabu na FIFA, na sisi tutachelewa kuisikiliza na pengine kuto uamuzi baada ya Januari, 2010 na hivyo Chelsea wanaweza kusajili Januari, 2010 kwani kawaida adhabu husimama hadi uamuzi wetu.”
Klabu ya Uswisi FC Sion ilikumbwa na mkasa kama wa Chelsea pale ilipomsajili Kipa wa Misri Essam El Hadary aliekuwa akichezea Al-Ahly na ikafungiwa kusajili na FIFA mwezi Aprili mwaka huu hadi 2010 lakini ikakata rufaa CAS na msimu huu imeruhusiwa kusajili kwani uamuzi wa rufaa yao utatoka baadae mwaka huu.
Kawaida jopo linalosikiliza Rufaa huko CAS huwa na Majaji wawili, mmoja atateuliwa na Chelsea na mmoja na FC Lenz, wakati Mwenyekiti wa Jopo ni toka CAS.
Uamuzi wowote wa CAS unaweza tu kukatiwa rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Uswisi tu na si pengine popote.
Mameneja wa Klabu Kubwa Ulaya wakutana Uswisi na UEFA
Kikao cha 11 cha Makocha Mahiri huko Ulaya pamoja na UEFA kinaendelea huko Nyon, Switzerland katika Jumba la Soka ya Ulaya na Mkurugenzi Mtendaji wa UEFA, Andy Roxburgh, amesema Kikao hicho ni kuwapa sauti Makocha na pia kuzungumzia masuala yanayohusu Marefa, Sheria, Mashindano na nini kinatokea Uwanjani.
Roxburg akaongeza: “Kikao hiki kinasaidia Makocha Vijana kujifunza kutoka kwa Makocha “Wazee” na wazoefu kama Sir Alex Ferguson. Sisi UEFA tumetoa jukwaa na Makocha wanatupa taarifa na vilevile wanajadiliana miongoni mwao.”
Kuhusu masuala ya Marefa, yupo aliekuwa Refa Mahiri sana, Pierluigi Collina, anaetoa ufafanuzi kwa Makocha kuhusu masuala yote ya Marefa.
Vilevile, Makocha hao walijulishwa rasmi uamuzi wa UEFA wa kufanya majaribio ya kutumia Marefa wawili wa ziada kwenye mechi yatakayofanyika msimu huu kwenye mashindano ya EUROPA LIGI kuanzia hatua ya Makundi. Marefa hao wawili watakuwa wakisimama karibu na Magoli, mmoja katika kila goli, ili kumpa ushauri Refa wa nini kinatendeka kwenye boksi.
Makocha waliohudhuria ni [kwenye Mabano Klabu zao:
Arsène Wenger (Arsenal FC), Sir Alex Ferguson (Manchester United FC), Manuel Pellegrini (Real Madrid CF), Jesualdo Ferreira (FC Porto), Claude Puel (Olympique Lyonnais), Ciro Ferrara (Juventus), Laurent Blanc (FC Girondins de Bordeaux), Didier Deschamps (Olympique de Marseille), Felix Magath (FC Schalke 04), Thomas Schaaf (Werder Bremen), Martin Jol (AFC Ajax), Valeri Gazzaev (FC Dynamo Kyiv), Walter Smith (Rangers FC), Dan Petrescu (AFC Unirea Urziceni), Abel Resino (Club Atlético de Madrid), Henk Ten Cate (Panathinaikos FC) and Bernard Challandes (FC Zürich).

No comments:

Powered By Blogger