Friday 4 September 2009

DEFOE AKERWA KUSIKIA JINA LA MICHAEL OWEN!!!
Mshambuliaji wa Tottenham, Jermain Defoe, ambae yumo kwenye Kikosi cha England ambacho Jumamosi kitacheza na Slovania mechi ya kirafiki Uwanjani Wembley, jijini London na Jumatano kipo hapohapo Wembley kwenye kinyang’anyiro cha kuingia Fainali Kombe la Dunia watakapopambana na Croatia, anakerwa jina lake kutajwa pamoja na Mshambuliaji wa Manchester United, Michael Owen.
Mara nyingi, kila Defoe anapochaguliwa Timu ya Taifa ya England, watu hutaja kuwa yeye ni mbadala wa Michael Owen ambae kwa mara nyingine tena hakuitwa Kikosini.
Defoe ametamka: “Owen ni Mchezaji mahiri. Lakini si kwamba mimi nipo England kwa sababu yeye hayupo! Hivyo hivyo si kwamba yeye akiwepo basi mie sipo!”
Kuna nadharia iliyojengeka kuwa Rooney, ambae panga pangua lazima yupo England, na Defoe hawawezi kucheza pamoja na mara nyingi akicheza Rooney basi pacha wake ni Emile Heskey. Hili limeota mizizi hasa ukichukulia kuwa katika magoli 10 Defoe aliyoifungia England hakuna hata moja alilofunga wakati yeye na Rooney wako uwanjani.
Lakini hilo halimtishi Defoe ambae amejibu: “Nishacheza na Rooney mara kadhaa. Ni Mchezaji stadi sana! Hupenda kumiliki sana mpira sawa na Robbie Keane tukicheza Tottenham na tumepata mafanikio makubwa! Sasa kucheza na Rooney, staili ni moja tu!”
HARGREAVES YUMO KIKOSI CHA MAN U UEFA!!
Kiungo wa Manchester United, Owen Hargreaves, miaka 28, ambae yuko nje ya Uwanja kwa mwaka mmoja sasa baada ya kuwa na matatizo ya magoti yake yote mawili na kufanyiwa operesheni huko Marekani, ni mmoja wa Wachezaji wa Manchester United waliokuwemo kwenye listi ya Kikosi kilichosajiliwa kwa ajili ya michuano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Mechi ya mwisho kwa Owen Hargreaves kuichezea Man U ilikuwa ni Septemba mwaka jana kwenye Ligi Kuu huko Stamford Bridge walipocheza na kutoka suluhu 1-1 na Chelsea.
Owen Hargreaves anatarajiwa kurudi Manchester Septemba 23 kutoka kwenye Kliniki ya Daktari Bingwa David Steadman ambae amewahi kuwafanyia na kuwatibu Wanamichezo mahiri akina Tiger Woods, Ruud van Nistelrooy, Alan Shearer na Michael Owen, Daktari ambae hatumui njia ya kupasua mtu kwa kisu bali hutumia utaalam wa hali ya juu kutoboa sehemu iliyoathirika na kutumia ‘ubongo’ wa mifupa ya Mchezaji mwenyewe kutibu majeruhi.
Manchester United wanaanza kampeni yao ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE hapo Septemba 15 kwa kucheza na Besiktas ugenini Ugiriki.

No comments:

Powered By Blogger