Benitez ang’oka Liverpool!!
Liverpool imethibitisha kuwa Rafa Benitez, ambae amedumu kwa Miaka 6, ataondoka Klabuni hapo baada ya makubaliano ya pande zote.
Baada ya Msimu mbovu uliokwisha Mwezi Mei, Benitez alijikuta yupo mashakani Timu ilipomaliza nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu na hivyo kuikosa nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Uhusiano wa Benitez na Wamiliki wa Klabu hiyo, Wamarekani wawili Tom Hicks na George Gillet, ulikuwa mbaya na walikuwa hawasikilizani.
Katika kipindi chake cha Miaka 6 hapo Liverpool, Benitez alifanikiwa kunyakua Klabu Bingwa Ulaya Mwaka 2005 na FA Cup Mwaka uliofuata lakini tangu wakati huo Liverpool imekuwa ikiambua patupu kila Msimu.
Akizungumza kwenye tovuti ya Liverpool, Benitez alitamka: “Nimesikitika sana kwamba mie si Meneja tena wa Liverpool na natoa shukrani zangu kwa Wafanyakazi na Wachezaji wote. Daima ntayaweka mema yote moyoni pamoja na mapenzi ya Washabiki. Sina maneno ya kusema ya kuwashukuru na ninajisikia fahari mno kusema nilikuwa Meneja wenu. Ahsanteni sana na daima kumbukeni: “Hamtatembea peke yenu!”
Kuondoka kwa Benitez kumezua utata kuhusu hatma ya Wachezaji Mastaa kama vile Nahodha wao Steven Gerrard, Fernando Torres na Javier Mascherano ambao wote wamekumbwa na uvumi mkubwa kuwa sasa milango yao ya kuondoka iko wazi.
Mbali ya utata wa Wachezaji kuondoka, pia haijajulikana nani atakuwa Mrithi wa Benitez hasa ukitilia maanani hata umiliki wa Klabu hiyo uko mashakani kwa vile wenye mali, Tom Hicks na George Gillet, wamekuwa kwa muda mrefu wakitafuta mnunuzi jambo ambalo limekuwa gumu kwa vile Klabu ina madeni makubwa.
No comments:
Post a Comment