Elton John afanya tamasha kuisaidia Watford
Gwiji la Muziki, Elton John, ambae aliwahi kuwa Mmiliki na pia Mwenyekiti wa Klabu ya Watford inayocheza Ligi Daraja la Coca Cola Championship, amefanya Tamasha maalum kuisaidia Watford kununua Wachezaji.
Tamasha hilo llifanyika Jumamosi iliyopita Uwanja wa Klabu hiyo uitwao Vicarage Road na llilingiza Pauni 600,000.Elton John alikuwa Mmiliki na Mwenyekiti wa Watford kati ya Mwaka 1976 na 1987.
Pia, Mwaka 2005 aliwahi kufanya Tamasha kama hilo kuchangia Watford.
Rio anahisi kalaanika!!
Nahodha wa England, Rio Ferdinand, ambae jana aliumia goti mazoezini huko Rusternburg, Afrika Kusini na hivyo kulikosa Kombe la Dunia linaloanza Juni 11, anahisi kama ‘amelaanika’ kwa kuumia huko.
Uchunguzi katika Hospitali moja huko Rusternburg umebaini kuwa anahitaji Wiki 4 hadi 6 ili kupona goti hilo. Mkasa huo kwa Rio unafuatia Msimu mzima wa Mwaka 2009/10 ulioisha Mei 9 ambao amekuwa akiandamwa na kuumia mara kwa mara kulikomfanya aichezee Klabu yake Manchester United Mechi 13 tu za Ligi Kuu.
Wakala wa Rio Ferdinand, Pini Zahavi, amesema Mteja wake amemwambia anahisi kama ‘amelaanika’ kwani haelewi kwa nini hilo limetokea.
Hata hivyo, Zahavi amesisitiza Rio, mwenye Miaka 31, ni Mtu imara na si ajabu akaibuka na kuichezea England Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2014 huko Brazil.
Essien aongeza Mkataba Chelsea
Michael Essien ameongeza nyongeza ya Miaka miwili katika Mkataba wake na Chelsea na atabaki Klabu hiyo hadi 2015.
Essien alijiunga na Chelsea Mwaka 2005 akitokea Lyon ya Ufaransa na ameshaichezea Klabu hiyo ya Stamford Bridge mechi 185 na kufunga mabao 22.
Kwa sasa Essien, Miaka 27, anauguza goti alililoumia katikati ya Msimu uliokwisha juzi wa Mwaka 2009/10 na maumivu hayo yamemfanya akose nusu ya pili ya Msimu wa Ligi Kuu England na pia ameshindwa kuichezea Ghana kwenye Fainali za Kombe la Dunia linaloanza Juni 11 huko Afrika Kusini ambapo Ghana ipo Kundi D pamoja na Ujerumani, Serbia na Australia.
Barca bado wana Fabregas!!
Rais wa Barcelona, Joan Laporta, bado ana imani kubwa Arsenal watamruhusu Cesc Fabregas ahamie kwao licha ya Ze Gunners kuipangua ofa yao wiki iliyopita.
Fabregas, mwenye Mkataba na Arsenal hadi 2015, ameshataja nia yake kurudi Barca alikoanzia kucheza Soka akiwa mtoto.
Inasemekana Arsenal waliikataa ofa ya Barca ya kumnunua Fabregas kwa Pauni Milioni 29 na Laporta amesema: “Hiyo ndiyo bei tunayoona ni thamani yake. Arsenal wameikataa na sasa ni juu yetu kuamua hatua inayofuata. Tunaongea nao.”
Laporta aliongeza kuwa wao walitaka wakubaliane na Arsenal kabla kuanza kwa Kombe la Dunia lakini wao hawana wasiwasi na wataendelea kuongea na Arsenal.
No comments:
Post a Comment