Capello na Mkataba mpya!
Wakati England leo ipo njiani kwenda Bondeni kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia, Meneja wao, Fabio Capello, amesaini Mkataba mwingine ambao una marekebisho yaliyoondoa kipengele cha kuruhusu yoyote kati ya pande mbili, yaani upande wa Capello na upande wa FA England, kuvunja Mkataba kabla ya muda wake kwisha hapo Mwaka 2012.
Marekebisho hayo sasa yatamfanya Capello abaki Kocha wa England hadi baada ya Fainali za EURO 2012 na hivyo kuondoa ile minong’ono kuwa yuko mbioni kwenda kumrithi Jose Mourinho huko Inter Milan mara tu baada ya Fainali za Kombe la Dunia.
Capello mwenyewe alikuwa amewaonya Wachezaji wake wa England wasiingize hatma zao za uhamisho toka Klabu zao wakati wapo kambini na England na hivyo kuathiri morali, kwa hivyo kwa yeye binafsi kusaini Mkataba mwingine kumeondoa kiwingu kichwani mwake.
Marekebisho hayo ya Mkataba pia yamethibitishwa na FA.
Boateng kuhamia Man City!
Beki wa Ujerumani, Jerome Boateng, ambae ni nduguye Kevin-Prince Boateng aliepata sifa mbaya ya kumng’oa Nahodha wa Ujerumani, Michael Ballack, toka Kombe la Dunia baada ya kumuumiza, amesema atasaini Manchester City kabla ya kuanza za Fainali za Kombe la Dunia ambalo yeye ni mmoja wa Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Ujerumani.
Boateng, mwenye miaka 21, na anaechezea Bundesliga na Klabu ya Hamburg, amethibitisha Kocha wa Man City, Roberto Mancini, alimfuata Hamburg na amemfanya akubali kuchezea Man City.
Boateng amesema amelazimika kuondoka Ujerumani baada ya Familia yao kuandamwa na Wanahabari baada ya nduguye kumuumiza Ballack kwenye Fainali ya FA CupChelsea ilipocheza na Portsmouth na hivyo kumfanya ashindwe kucheza Kombe la Dunia.
Jerome Boateng huenda akakumbana na Kevin-Prince Boateng kwenye Kombe la Dunia baada ya Kevin-Prince kuamua kuichezea Ghana, ambayo ni Nchi ya Baba yake, kwa vile Ujerumani na Ghana zipo Kundi D pamoja.
Jerome Boateng amelalamika: “Inanisumbua jinsi Familia yetu inavyoandamwa! Nyumbani kwetu mlangoni wamejazana Wapiga Picha na hatuwezi hata kutoka nje! Nimejaribu kuwaita Polisi lakini wanasema hawana la kufanya na inabidi tuikubali hali kwa vile sisi ni Boateng! Hii imefika mbali!”
No comments:
Post a Comment