Arsenal wamekataa kusikiliza ofa ya FC Barcelona ya kutaka kumnunua Nahodha wao Cesc Fabregas na wamesisitiza wao hawana nia ya kumhamisha Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Spain alie njiani kwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia na Nchi yake.
Inadaiwa Barcelona waliwasilisha ofa rasmi ya kumnunua Fabregas hapo juzi.
Fabregas, miaka 23, alizungumza wiki iliyopita na kudai kuwa yupo na nia ya kurudi Barcelona alikoanzia Soka lake akiwa mtoto.
Arsenal imeikataa ofa hiyo ya Barcelona na imetangaza kwenye tovuti ya Klabu hiyo kwamba Mchezaji huyo ana Mkataba hadi 2015 na ni muhimu na anathaminiwa sana na Ze Gunners.
Grant kutua West Ham
Bosi wa zamani wa Portsmouth na Chelsea Avram Grant huenda leo akatangazwa Meneja mpya wa West Ham kuchukua nafasi ya Gianfranco Zola aliefukuzwa.
Grant aliondoka Portsmouth, Timu iliyoshushwa Daraja, hapo Mei 21 na inasemekana amekatiza vakesheni yake ili aende London kukamilisha taratibu za kutua West Ham.
Wamiliki wa pamoja wa West Ham, David Sullivan na David Gold, wamekubaliana kuhusu uteuzi wa Grant ambae alipokuwa Chelsea aliiwezesha kufika Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI lakini ikabwagwa na Manchester United na pia aliifikisha Portsmouth Fainali ya FA Cup lakini ikafungwa na Chelsea.
‘WAKOMBOZI WEKUNDU’ wabwaga manyanga Man United!!!
Kile Kikundi cha Mashabiki Matajiri waliokubuhu wa Manchester United, maarufu kama ‘Wakombozi Wekundu’, waliokuwa na nia ya kuinunua Man United kutoka kwa Wamiliki wake, Familia ya Kimarekani ya Glazer, wamesimamisha azma yao ya kutoa ofa ya ununuzi wa Klabu hiyo.
Kundi hilo limedai thamani ya Klabu hiyo imepotoshwa mno na Vyombo vya Habari na azma yao pia imepindishwa na hivyo kulifanya zoezi lao lipata upinzani.
Wiki iliyopita, Familia ya Glazer, ilitangaza kuwa hawana nia ya kuiuza Manchester United ambayo waliinunua Mwaka 2005 kwa Pauni Milioni 800.
Mbali ya Kundi hilo la Matajiri, ‘Wakombozi Wekundu’, Familia hiyo ya Glazer imekuwa ikipingwa na Kundi la Mashabiki wanaojiita MUST [The Manchester United Supporters Trust] waliokuwa wakiendesha kampeni kwa kuwataka wafuasi wao wavae sare za rangi ya Kijani na Dhahabu hizo zikiwa ndizo rangi za Klabu anzilishi ya Man United, Newton Heath, iliyoanzishwa Mwaka 1878 na Wafanyakazi wa Depo ya Reli.
No comments:
Post a Comment