Sunday 14 June 2009

Afrika Kusini 0 Iraq 0
Katika mechi ya ufunguzi ya Mashindano ya kugombea Kombe la Mabara la FIFA, Wenyeji Afrika Kusini leo wametoka sare ya 0-0 na Mabingwa wa Asia Iraq katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Ellis Park, mjini Johannesburg.
Timu hizi zipo KUNDI A pamoja na Spain na New Zealand ambao watacheza baadae leo kuanzia saa 3 na nusu usiku, saa za bongo, kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng huko Rustenburg.
VIKOSI:
AFRIKA KUSINI: KHUNE, GAXA, MASILELA, MOKOENA, MHLONGO, SIBAYA, MODISE, DIKGACOI, BOOTH, PARKER, FANTENI.
IRAQ: MOHAMMED K., MOHAMMED ALI, BASIM, FAREED, NASHAT, IMAD, YOUNUS, KARRAR, SALAM, ALI HUSSEIN, MAHDI
VIDIC ASEMA SING’OKI MAN U NG’O!!!!
Beki wa Manchester United Nemanja Vidic ametupilia mbali uvumi kwamba anaelekea Spain kujiunga na Real Madrid au Barcelona kwa kutamka wazi wazi kuwa hana nia ya kuhama kwenda kokote.
Vidic ametamka: ‘Nina furaha hapa na msimu ujao tunaanza upya! Sina nia ya kwenda kokote!’
Vidic amesistiza kuwa msimu ujao Manchester United inataka kuweka historia mpya kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya 4 mfululizo.
REFA WA LIGI KUU ASTAAFU!!!
Rob Styles, mmoja wa Marefa wa Ligi Kuu England ambae siku zote utata humwandama kila anapochezesha mechi, amestaafu kuwa Refa na habari hizi zimethibitishwa na Bodi ya Marefa wa Kulipwa.
Rob Styles, mwenye umri wa miaka 45, amekuwa akiandamwa na malalamiko mengi kutoka Klabu za Ligi Kuu kutokana na maamuzi yake yenye utata.
Msimu uliokwisha Mameneja kadhaa walilalamika na Gary Megson wa Bolton Wanderers alipiga kelele mno pale Rob Styles alipoipa Manchester United penalti baada ya Jlloyd Samuel wa Bolton kuucheza mpira kihalali kabisa na Styles akaamua alimchezea faulo Ronaldo wakati hakumgusa.
Katika mechi nyingine inadaiwa aliipa Chelsea penalti yenye utata walipocheza na Liverpool mwanzoni mwa msimu wa 2007/8.
Inadaiwa lawama hizo za mara kwa mara pamoja na kutopewa mechi kubwa kuchezesha kumemfanya akate tamaa na kuamua kustaafu. Mechi yake pekee kubwa aliyochezesha ni Fainali ya Kombe la FA mwaka 2005.

No comments:

Powered By Blogger