Tuesday, 16 June 2009

FIFA yatupilia mbali malalamiko ya Misri!!!
Jioni hii FIFA imewaandikia Chama cha Soka cha Misri kuhusu malalamiko yao juu ya mechi ya jana kati ya Brazil na Misri hasa uamuzi wa Refa Howard Webb wa Uingereza wa kuwapa penalti Brazil baada ya kuashiria ni kona.
FIFA walipokea barua ya malalamiko toka kwa Misri mara baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Free State huko Mangaung, Bloemfontein.
Misri hawakupinga uamuzi wa Refa Howard Webb kutoa penalti kwa Brazil na kumpa Kadi Nyekundu Mlinzi wao Ahmed El-Mohamadi, walichokipinga kilikuwa ni jinsi Refa huyo alivyofikia uamuzi huo baada ya kwanza kuamua ipigwe kona.
FIFA imeelezea kwenye barua yao kuwa baada ya kuchunguza ushahidi wote ukiwa pamoja na Ripoti ya Mechi ya Refa Howard Webb na maelezo ya ziada kutoka kwa Refa huyo, imeridhika kuwa uamuzi wa kutoa penalti na Kadi Nyekundu ulifikiwa baada ya Refa Howard Webb kushirikiana vyema na Mike Mullarkey aliekuwa Mshika Kibendera, au tumwite Msaidizi wa Refa kama ipasavyo siku hizi, ambaye pia alithibitisha kila kitu kilichosemwa na Refa Howard Webb.
Tukio hilo la utata lilitokea dakika za majeruhi huku mechi ikiwa 3-3 na katika kizaazaa golini mwa Misri Beki El-Mohamadi akaokoa mpira akiwa kwenye mstari wa goli kwa mkono na kisha kujidondosha chini, akishika kichwa na kuvunga kaumia. Refa Howard Webb alionekana waziwazi akitoa kona na Wachezaji wa Brazil wakamzonga wakilalamika na kutoa ishara mpira umeshikwa kwa mkono.
Wakati huo El-Mohamadi alikuwa kajigalagaza chini na, pengine, hapo ndipo Refa Howard alipoambiwa yule Beki wa Misri aliushika mpira.

No comments:

Powered By Blogger