Monday 15 June 2009

Klabu za Spain kuendelea 'kupora' England???
  • Alonso, Mascherano kuhama?

  • Fabregas kurudi 'nyumbani' Barca?
Wakati Cristiano Ronaldo yuko njiani kutimiza ‘ndoto yake’ ya kucheza Spain Klabuni Real Madrid, Klabu nyingine za Ligi Kuu England zimetangaza vita ya kujihami ili wasiporwe Mastaa wao na Klabu za Spain hasa Real Madrid na Barcelona.
Liverpool imebidi itangaze waziwazi Xabi Alonso na Javier Mascherano hawauzwi kwa bei yeyote ile baada ya kuibuka habari nzito kutoka Spain kuwa na wao wako njiani kuhama Anfield kwenda Spain.
Mchezaji wa Kimataifa wa Argentina, Mascherano, inasemekana anapata shinikizo kubwa kutoka kwa Mkewe wahamie Spain na hasa Barcelona wakati Alonso anaunganishwa na Real Madrid huku Rais wa Real Florentino Perez akionyesha kila dalili Alonso yuko kwenye listi yake ya ‘manunuzi’.
Taarifa hizo za kuhama kwa Alonso na Mascherano zimezagaa mno kiasi Klabu ya Liverpool imebidi itoe taarifa rasmi kwenye tovuti yake inayosema: ‘Ingawa kuna taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari kuhusu uhamisho wa Xabi Alonso na Javier Mascherano, Liverpool haijapokea ombi lolote rasmi au ofa yeyote kutoka Klabu yeyote kuhusu Wachezaji hao. Hata hivyo wote hawauzwi na Liverpool pia haina nia ya kuchukua Mchezaji yeyote kutoka Spain.’
Nae Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, amedokeza kuwa endapo Pep Guardiola, Meneja wa Barcelona, atamtafuta yeye basi atachukulia hilo kama kitu ‘spesho!’
Hata hivyo, Fabregas pia amedokeza kuwa kwa sababu yeye ni Nahodha wa Arsenal ni jukumu lake kuhakikisha Klabu yake inatwaa Vikombe.
Kauli hizi za utata zinaendelea kuwachanganya Wadau na kuzipa uzito taarifa kuwa Fabregas nae yuko njiani kurudi Barcelona Klabu aliyoanzia tangu kiwa kijana mdogo sana.

No comments:

Powered By Blogger