LIGI KUU England kuanza Agosti 15, Ratiba kutoka Jumatano!!!!
Ule uhondo, utamu, mashamushamu, mijadala, ngonjera, mabishano na hata masumbwi yanayoletwa na starehe kubwa ya LIGI KUU ENGLAND kwa Wadau wengi yataanza kuonekana kwenye kila kijiwe kuanzia tarehe 15 Agosti 2009 pale msimu mpya wa mwaka 2009/10 utakapoanza.
Msimu huu utamalizika tarehe 9 Mei 2010.
Na kama kawaida Msimu mpya hutanguliwa na ile mechi ya Fungua Pazia ambayo huchezwa wiki moja kabla msimu kuanza kwa kugombea NGAO YA HISANI kati ya Bingwa wa LIGI KUU na Bingwa wa Kombe la FA.
Kwa hivyo, Manchester United, kama Bingwa wa LIGI KUU, atachuana na Chelsea, anaeshikilia Kombe la FA tarehe 9 Agosti 2009 Uwanjani Wembley mjini London.
Ratiba ya msimu huu mpya wa 2009/10 itatolewa rasmi Jumatano tarehe 17 Juni 2009.
Uandaaji wa ratiba hii, huku ukisaidiwa na teknolojia ya kisasa kabisa ya kutumia kompyuta , umechukua karibu mwezi mzima na ulianza tu mara baada ya kujulikana ni Timu zipi zimepanda Daraja kuingia Ligi Kuu hasa ukizingatia mbali ya Timu 2 zilizopanda Daraja moja kwa moja kwa kumaliza nafasi za kwanza na za pili, Timu hizo zikiwa ni Wolverhampton Wanderers na Birmingham, Timu ya 3 kupanda Daraja ilikuwa kwenye kinyanga’nyiro maalum kilichoshirikisha Timu zilizoshika nafasi ya 3, 4, 5 na 6 ili kupata Timu moja na Burnley ikaibuka kidedea.
Baada ya hapo, Wasimamizi wa Ligi Kuu na wale wa Ligi za Chini ikabidi wakutane ili wapambanue Timu zinazotoka maeneo mamoja, hata kama wako Madaraja tofauti, wote hawachezi nyumbani siku moja.
Hii ni kwa sababu ya kiusalama na kuzuia misongamano.
Hivyo, Timu kama vile Aston Villa na Wolverhampton walio Ligi Kuu wanaweza kupangiwa kucheza nyumbani na wenzao wa eneo moja Birmingham City na West Brom Albion, iliyo Daraja la Chini, lazima wacheze ugenini.
Sababu nyingine zinazozingatiwa katika upangaji ratiba ni kama:
-Klabu hazipangiwi, bila sababu maalum, mechi zaidi ya mbili mfululizo za nyumbani tupu au ugenini tupu.
-Mwanzoni mwa ligi na mwishoni mwa ligi ni lazima Klabu zicheze kwa mpangilio wa mechi moja nyumbani na inayofuata ugenini ili kuleta usawa na ushindani bora.
-Klabu inayocheza ugenini siku ya Krismasi lazima iwe nyumbani siku ya Mwaka mpya au kinyume chake. Katika siku hizo za Sikukuu mechi za Wapinzani wa Jadi, kama vile Man U v Liverpool, Liverpool v Everton, Man U v Man City nk., hazipangwi.
Mbali ya vitu vya msingi kama hivyo Polisi na Viongozi wa Miji ya kila Klabu hushirikishwa ili kutoa michango yao na maoni na kitu kikubwa, mara nyingi, kwa sababu ya kiusalama, Bigi Mechi, kama vile Man U v Liverpool, huchezwa mchana kweupe jua likiwa ‘utosini’ kwa sababu za kiusalama.
No comments:
Post a Comment