Sunday, 14 June 2009

LEO NI MABARA BONDENI!!
South Africa v Iraq
KUNDI A, KIWANJA: Ellis Park, Johannesburg SAA: 11 JIONI [BONGO]
Wenyeji, Afrika Kusini, wakiongozwa na Nahodha Aaron Mokoena aliyekuwa Blackburn Rovers lakini msimu ujao atachezea Portsmouth watafungua dimba na Mabingwa wa Asia Iraq.
Kikosi cha Afrika Kusini kina Wachezaji Wachezaji wengine wanaochezea Ligi Kuu England ambao wanategemewa kuanza hivi leo nao ni Steven Piennaar wa Everton na Mchezaji mpya wa Blackburn Rovers Elrio van Heerden.
Kikosi cha Iraq inasemekana kipo kamili bila majeruhi na ni pamoja Kiungo Nashat Akram ambae amenunuliwa na FC Twente ya Uholanzi na ataonekana rasmi msimu ujao.
Mchezaji wao mwingine ambae ameshawahi kucheza Ulaya ni Hawar Mulla Mohammed.
Kwa Afrika Kusini hii ni nafasi nzuri sana kujizoeza na mikimiki ya Kombe la Dunia ambalo mwakani wao ni Wenyeji. Meneja wa Afrika Kusini ni Mbrazil Joel Santana.
Pamoja na Iraq, Afrika Kusini wako Kundi moja na Spain na New Zealand.
Iraq wameingia Mashindano haya kwa sababu ni Mabingwa wa Asia lakini kwa mwaka mmoja Timu imekuwa ikisuasua na hawajashinda mechi yeyote kwa mwaka mzima sasa na ni hivi karibuni tu ndio wameteua Kocha kutoka Serbia, Bora Milutinovic, ambae amewahi kusimamia Nchi 5 tofauti kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Afrika Kusini na Iraq hawajahi kukutana hata mara moja. Kwa Afrika Kusini hii ni mara ya pili kushiriki Kombe la Mabara mara ya kwanza ikiwa mwaka 1997 walipotolewa hatua ya Makundi baada ya kutoka suluhu mechi moja na kufungwa 2.
Refa: Hany Abu Rida (Egypt)
Wasaidizi: Karoly Torok (Hungary), Vincent Monnier (Switzerland)
Spain v New Zealand
KUNDI A, KIWANJA: Royal Bafokeng Stadium, Rustenburg SAA 3 NA NUSU USIKU [BONGO]
Mabingwa wa Ulaya, Spain, ambayo ndio Timu nambari Wani kwa ubora kwenye listi ya FIFA wanaingia uwanjani kupambana na Mabingwa wa Nchi za Baharini [Oceania] New Zealand huku Spain wakiwakosa nyota Andres Iniesta na Marcos Senna ambao ni majeruhi.
Lakini Mastaa wao wengine waliokuwa hatihati kutoonekana kwa maumivu sasa wamepona na wanategemewa kucheza. Nao ni kama Carles Puyol, Sergio Ramos, David Silva, Santi Carzola, Gerard Pique na Sergi Busquets.
New Zealand watamkosa Nahodha wao Ryan Nelsen, anaechezea Blackburn Rovers, aliechanika musuli ya mguu. Hata hivyo Mchezaji wa zamani wa Fulham, Simon Elliott na yule wa Celtic, Chris Killen, watakuwepo.
Spain wako Afrika Kusini chini ya Meneja wa zamani wa Real Madrid, Vicente del Bosque, alieichukua Timu baada ya EURO 2008 na tangu wachukue EURO 2008 hawajafungwa katika mechi 10 sasa.
Hii ni mara kwanza kwa Spain kushiriki Kombe la Mabara.
New Zealand, walio chini ya Meneja Ricki Herbert, ni mara yao ya 3 kucheza Kombe la Mabara lakini hawajahi kuambua hata pointi moja mara zote za nyuma.
Kabla ya kutua Afrika Kusini, Ne Zealand walicheza mechi ya moja ya kirafiki mjini Dar es Salaam, Tanzania na kufungwa 2-1 na Tanzania, kisha wakatoka suluhu na Botswana na wakafungwa na Mabingwa wa Dunia, Italy, 4-3 siku ya Jumatano huko Afrika Kusini.
Spain na New Zealand hawajahi kukutana uso kwa uso ingawa katika Fainali za Kombe la Dunia la Vijana wa chini ya miaka 17, Spain waliikung’uta New Zealand mabao 13-0.
Refa: Coffi Codjia (Benin)
Wasaidizi: Komi Konyoh (Togo), Alexis Fassinou (Benin)

No comments:

Powered By Blogger