Thursday 16 July 2009

Adebayor aomba muda zaidi kutafakari uhamisho kwenda Man City!!!
Emmanuel Adebayor ameomba apewe muda zaidi kutafakari uhamisho wake kutoka Arsenal kwenda Manchester City kwa sababu anahofia lawama kubwa atakazopata nyumbani kwao Togo ambako Arsenal ni moja ya Klabu zinazopendwa sana.
Arsenal imeshakubali ofa ya Pauni Milioni 25 toka kwa Man City kumnunua Mshambuliaji huyo ambae tayari ameshapewa Kibali cha kubadili Mwajiri wa Kazi.
Hata hivyo inaaminika mapenzi ya Adebayor ni kuhamia AC Milan na huenda kusita kwake kuhamia Man City ni kupata muda zaidi ili mipango ya kwenda AC Milan isukike vizuri.
Man U huenda ikanunua Wachezaji zaidi!
Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United, David Gill, amesema Klabu yake inaweza kununua Wachezaji kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa mwishoni mwa Agosti.
Kufuatia kuondoka kwa Ronaldo na Tevez, wengi walitegemea Man U itaingia sokoni kwa kishindo lakini hadi hii leo Mabingwa hao wamewanunua Luis Antonio Valencia, Michael Owen na Gabriel Obertan kwa dau lisilozidi Pauni Milioni 20 kwa Wachezaji wote.
Mwanzoni mwa wiki hii, Sir Alex Ferguson, Meneja wa Man U, alisema hawana mpango wa kununua Mchezaji yeyote kwa vile soko limeota mbawa na thamani za Wachezaji zimebomoa paa.
Hata hivyo Bosi mkubwa David Gill, kabla ya Mabingwa hao kuanza ziara ya Asia, hakufunga milango na amekiri bado wanashughulikia ishu ya uhamisho. Gill amesema: ‘Nitaanza siku yangu kila siku kwa kufungua barua pepe na mawasiliano mengine na nina uhakika kutakuwa na masuala ya uhamisho wa Wachezaji!’

No comments:

Powered By Blogger