Tuesday 14 July 2009

Baada ya kumnasa Tevez, Man City wapo mezani kuhusu Adebayor
Manchester City wako kwenye majadiliano mazito ili kumnasa Mshambuliaji kutoka Togo anaecheza Arsenal Emmanuel Adebayor mara tu baada ya Carlos Tevez kumwaga wino kwa Mahasimu hao wa Manchester United.
Inaaminika Adebayor, miaka 25, anaweza akachukuliwa na Man City kwa Pauni Milioni 25 baada ya kuichezea Arsenal kwa miaka mitatu na nusu akitokea Monaco ya Ufaransa.
Adebayor msimu uliokwisha aliifungia Arsenal mabao 16 na kujiunga kwake na Man City kutaimarisha Kikosi hicho ambacho tayari kishawabeba Washambuliaji Carlos Tevez, Roque Santa Cruz na Kiungo Gareth Barry.
Vilevile, Kikosi hicho cha Meneja Mark Hughes kinaweza kuimarika zaidi kwani pia kuna habari nzito Nahodha wa Chelsea na England, John Terry, anaishinikiza Klabu yake imruhusu afanye mazungumzo na Man City ili kuona uwezekano wa kuhama ingawa mpaka sasa hakuna kilichotamkwa.
Kwa kumsaini, Emmanual Adebayor, Mchezaji aliehamia Arsenal kutoka Monaco kwa Pauni Milioni 7 tu, Mark Hughes ana uhakika wa kupata huduma bora ya ufungaji magoli kwani Adebayor katika mechi 142 alizochezea Arsenal amepachika mabao 62.
Msimu wa mwaka 2007/8, Adebayor aliifungia Arsenal mabao 30 lakini msimu uliokwisha majeruhi ya mara kwa mara yamemfanya afunge goli 16 tu kitu kilichowafanya Mashabiki wa Arsenal wahoji moyo wake kwa Klabu.
Kuhama kwa Adebayor hakumstui sana Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ambae tayari ameshamweka sawa Mshambuliaji kutoka Morocco, Marouane Chamakh, anaecheza Bordeaux ya Ufaransa, kuziba pengo hilo.

No comments:

Powered By Blogger