Sunday 12 July 2009

John Terry amwomba kibali Abramovich ili aongee na Man City
Kuna taarifa nzito kuwa jana usiku Nahodha wa Chelsea John Terry na Mwenye Klabu hiyo Roman Abramovich walikuwa kwenye mazungumzo mazito ili kuamua hatima ya Terry baada ya Mchezaji huyo kuomba apewe kibali ili azungumze na Manchester City ambao wanamtaka Sentahafu huyo kwa udi na uvumba.
Manchester City, Klabu inayomilikiwa na Matajiri waliokubuhu kutoka Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu wanaotoka Koo za Kifalme za huko, inasadikiwa wako tayari kutoa dau la Pauni Milioni 50 kumnunua Terry na pia kumpa mshahara wa Pauni Laki 2 na nusu kila wiki kitita ambacho kitamfanya awe Mchezaji mwenye mshahara mkubwa Uingereza yote.
Terry, mwenye miaka 28, ambae amekuwa Chelsea tangu utotoni, anaichukulia nafasi hii kama karata yake ya mwisho na hategemei kuipata tena.
Mpaka sasa haijajulikana nini kiliamuliwa katika mazungumzo hayo kati ya Tajiri na Mchezaji wake.
Ibrahimovic adai Chelsea inamtaka!!
Mshambuliaji kutoka Sweden anaecheza Inter Milan, Zlatan Ibrahimovic, amedai kuwa Klabu ya Chelsea inataka asaini huko ingawa Klabu yake inagoma kuwa Mchezaji huyo haendi kokote.
Mwenyewe Ibrahimovic hakusema moja kwa moja kama yuko tayari kuhamia Chelsea ingawa amekubali kuwa ikifika hatua ya uamuzi basi yuko tayari kutafakari kwa undani kama Ligi Kuu England inamfaa na Klabu ipi ni bora kwake.
Mbali ya Chelsea, Ibrahimovic pia amevumishwa kuwa Manchester United wanamuwinda ingawa si yeye wala Manchester United waliothibitisha habari hizo.

No comments:

Powered By Blogger