Thursday 16 July 2009

Fainali Copa Libertadores: Cruzeiro 1 v Estudiantes 2
Estudiantes ya Argentina imenyakua Ubingwa wa Klabu za Marekani ya Kusini ugenini baada ya kuifunga Cruzeiro ya Brazil 2-1 katika mechi ya marudiano ya Fainali ambayo ni ya 50 ya Mashindano hayo maarufu kwa jina la COPA LIBERTADORES baada ya Klabu hizo kutoka suluhu 0-0 kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa wiki iliyokwisha.

Fainali hii ilichezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Cruzeiro walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Henrique dakika ya 52 lakini Estudiantes walisawazisha dakika ya 58 kupitia Gasto Nicolas Fernandes na Mauro Boselli akawapa Ubingwa kwa bao la dakika ya 73.
Man U waanza ziara bila Vidic!!
Nemanja Vidic hayumo kwenye Kikosi cha Manchester United kilichopanda ndege leo kuelekea Malaysia, Korea na China.
Mwezi uliokwisha Vidic alijitoa kwenye Kikosi cha Timu ya Taifa ya Serbia kilichopambana na Visiwa vya Faroe kwenye mechi ya Makundi kuwania kuingia Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuumia enka na inasadikiwa kuachwa kwake kusafiri ni kumpa muda zaidi wa kuuguza hiyo enka.
Mchezaji mwingine ambae hakuwemo kwenye msafara huo ni Chipukizi Rafael Da Silva.
Lakini, majeruhi wa muda mrefu, Wes Brown na Gary Neville, walikuwemo pamoja na Wachezaji wapya Michael Owen, Antonio Valencia na Gabriel Obertan.
Man U wanacheza na Kombaini ya Malaysia Jumamosi, siku mbili baadae watacheza na FC Seoul huko Korea na tarehe 26 Julai watacheza China na Hangzhou Greentown.
Kikosi kamili kilichosafiri ni: Edwin van der Sar, Tomasz Kuszczak, Ben Foster, Jonny Evans, Patrice Evra, Rio Ferdinand, Gary Neville, Wes Brown, John O’Shea, Fabio da Silva, Nani, Zoran Tosic, Darren Fletcher, Anderson, Darron Gibson, Paul Scholes, Michael Carrick, Ryan Giggs, Michael Owen, Dimitar Berbatov, Federico Macheda, Wayne Rooney.
Benitez aota kubeba Ubingwa LIGI KUU England!!
Bosi wa Liverpool, Rafa Benitez, amekiri ili Timu yake ichukue Ubingwa wa Ligi Kuu England inabidi wasifanye kosa lolote na kupoteza mechi yeyote.
Liverpool msimu uliokwisha walimaliza Ligi wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Mabingwa Manchester United na kuambua jumla ya pointi 86 huku Manchester United wakichota pointi 90.
Liverpool wanahaha kuumaliza ukame wa miaka 20 wa kutotwaa Ubingwa ingawa Benitez anaamini ana Kikosi imara kupita vyote vya nyuma lakini bado ana wasiwasi wanahitaji kuboreka zaidi.
Benitez amesema: ‘Inabidi ufanye kila kitu sahihi huwezi kukubali kufungwa mechi nyingi! Chelsea, Man U na Arsenal ni Timu ngumu na msimu huu Tottenham, Aston Villa na Man City zitatoa upinzani! Ni Ligi ngumu!’
Moyes: ‘Lescott hauzwi!’
Meneja wa Everton, David Moyes, amesisitiza Mlinzi wake anaechezea England, Joleon Lescott hauzwi baada ya kuandamwa mfululizo na Klabu tajiri Manchester City.
Akiongea kwenye mkutano na Wadau wa Klabu hiyo, Moyes amesema: ‘Nilishasema hakuna Mchezaji atakaeuzwa hapa Everton na sina haja kurudia hilo!’
Msimamo huo wa David Moyes umeungwa mkono na Mwenyekiti wa Everton, Bill Kenwright, aliesema David Moyes ndie mwenye kauli
ya mwisho kuhusu Wachezaji.

No comments:

Powered By Blogger