Tuesday 9 June 2009

AC MILAN YASEMA KAKA KAUZWA REAL MADRID!!!
· DAU NI REKODI DUNIANI!!!!

Klabu ya Serie A Italia, AC Milan, jana imethibitisha kupitia tovuti yake kuwa Mchezaji wao Nyota kutoka Brazil Kaka, umri miaka 27, ameuzwa kwenda Klabu ya Real Madrid ya Spain bila ya kutaja kiasi gani kilitumika kumnunua na habari hizi zikathibitishwa na Real Madrid ambao nao walitoa tamko kupitia tovuti yao kwamba Kaka sasa ni Mchezaji wao na ameshafaulu upimaji wa afya na atakuwa Klabu hiyo kwa mkataba wa miaka 6.
Kaka alizaliwa Brasilia, Brazil tarehe 22 Aprili 1982 na jina lake kamili ni Ricardo Izecson dos Santos Leite lakini anaitwa Kaka kwani huko Brazil mtu anaeitwa Ricardo kifupisho chake maarufu ni ‘Kaka’.
Ingawa dau halikutangazwa rasmi lakini inaaminika ni Pauni Milioni 56 na hiyo itakuwa ni rekodi ya dunia kumnunua Mchezaji na itavunja ile rekodi ya mwaka 2001 ambayo pia Real Madrid waliiweka walipomnunua Zinedine Zidane kwa Pauni Milioni 45.6.
Kaka alijiunga na AC Milan mwaka 2003 akitokea Klabu ya Sao Paolo ya Brazil kwa dau kiduchu la Pauni Milioni 8.5 na akapata mafanikio makubwa akiwa na klabu hiyo ya Italia.
Mwaka 2007, Kaka pamoja na AC Milan, walishinda UEFA CHAMPIONS LEAGUE, UEFA SUPER CUP, FIFA WORLD CUP na Timu yake ya Taifa ya Brazil, Kaka akiwemo, ilinyakua FIFA CONFEDERATION CUP na mafanikio hayo yote, mwaka huo 2007, yakamvisha Kaka Taji la MCHEZAJI BORA DUNIANI la FIFA.
Kaka ameshawahi kushinda Serie A akiwa na AC Milan na alikuwa kwenye Kikosi cha Brazil kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 2002.
Mwezi Januari, Klabu ya LIGI KUU England, Manchester City, ilitaka kumnunua Kaka kwa dau la Pauni Milioni 100 na ilitoa ofa ya Mshahara wa juu kuliko wa Mchezaji yeyote duniani ulioripotiwa kuwa ni Pauni Laki 5 kwa wiki, lakini Kaka mwenyewe akaamua kubaki AC Milan.
Kwa sasa Kaka yuko kambini na Timu ya Taifa ya Brazil huko kwao Brazil na Jumatano inacheza mechi ya mchujo kuwania nafasi kuingia Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 dhidi ya Paraguay mechi iatakayochezwa Recife, Brazil.
Mara baada ya mechi Kaka na Brazil wataelekea Afrika Kusini kushiriki Kombe la Mabara la FIFA [FIFA CONFEDERATION CUP] linaloanza Juni 14.

No comments:

Powered By Blogger