Tuesday 9 June 2009

ULAYA-Nani kuungana na Uholanzi Bondeni?
Kesho Barani Ulaya kuna mechi 7 kutoka Makundi tofauti matano yanayogombea nafasi za kufuzu kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010 lakini mechi hizo zote za Jumatano tarehe 10 Juni 2009 haziwezi kutoa Nchi yeyote itakayojumuika na Uholanzi, Australia, Japan na South Korea ambazo tayari zimeingia Fainali Afrika Kusini 2010.
Kila Nchi zilizo kwenye Makundi yanayocheza kesho bado wana vita ingawa kwa baadhi kuna ahueni fulani na wengine wanagombea kupenya kwenda Bondeni kwa kupata nafasi ya pili.
Ulaya kuna Makundi 9 na Washindi wa kila Kundi watateremka moja kwa moja Bondeni huku Washindi wa pili wanane wenye matokeo bora watapigiwa dro maalum ili kucheza mechi za nyumbani na ugenini kupata Nchi 4 zitakazoshuka Bondeni.

-Nini kina mvuto kesho?
Kundi la 9 linaongozwa na Ujerumani wenye pointi 16 lakini wamecheza mechi moja zaidi ya Finland, wenye pointi 10, na Urusi, wenye pointi 12.
Kesho Finland na Urusi wanapambana.
Wadau watakumbuka Meneja wa Urusi ni Guus Hiddink ambae hivi juzi tu akifanya kibarua cha muda huko Stamford Bridge aliiwezesha Timu ya rafiki yake Roman Abramovitch, Chelsea, ichukue FA CUP.
-Mechi nyingine
Kundi la 1 kuna Sweden ambao wanaonekana kudebweda hasa baada ya Jumamosi kupigwa kwao na Watani wao wa Jadi Denmark bao 1-0.
Kundi hili Denmark ndio vinara wakiwa na pointi 16, Hungary ni wa pili pointi 13, wakifuata Ureno pointi 9 na Sweden pointi 6.
Kundi la 6, England wanabembea kwa kuongoza wakiwa na pointi 18 baada ya kushinda mechi zao zote 6. Croatia ni wa pili wakiwa na pointi 11 lakini Belarus wako nafasi ya 3 na pointi 9 na wamecheza mechi moja pungufu.
Kundi la 7 wanaongoza Serbia na kesho watacheza na ‘vibonde’ Faroe Island na kila mtu anategemea watashinda na kuongoza Kundi hili kwa pointi 8 ingawa watakuwa wamecheza mechi mbili zaidi ya Ufaransa wanaowafukuza.
Katika Kundi la 9, ingawa Uholanzi tayari imetua Bondeni, kesho watakuwa wenyeji wa Norway ambao kwenye Kundi hili hawajashinda hata mechi moja!
-Takwimu
Kwa wale Mashabiki wa Takwimu, England ndio inayoongoza Ulaya kwa kufunga Magoli 20 katika mechi 6 wakifuatiwa na Ujerumani goli 18 na Slovakia goli 17.
Mabingwa Watetezi wa Dunia, Italia, ingawa wanaongoza Kundi lao la 8, wamefunga goli 9 tu katika mechi 6 walocheza.


Scolari ahamia kwa Mabingwa wa Uzbekistan
Meneja wa zamani wa Chelsea, aliewahi kuwa pia Meneja wa Brazil Luiz Felipe Scolari, amepata kibarua kipya huko Uzbekistan akiwa Bosi wa Mabingwa wa Nchi hiyo Klabu inayoitwa Bunyodkor.
Scolari, miaka 60, alietimuliwa Chelsea mwezi Februari mwaka huu, amepata kazi hapo Bunyodkor kwa mkataba wa miezi 18 na anamrithi Mbrazil mwenzake, Zico, aliewahi kuwa Supastaa mkubwa Brazil na duniani, alieifanikisha Klabu hiyo kutwaa Ubingwa, Kombe la Uzbekistan pamoja na kuifikisha Nusu Fainali ya klabu Bingwa Asia.
Zico ameondoka Bunyodkor kwenda Urusi mwezi Desemba mwaka jana ili kuwa Meneja wa CSKA Moscow

No comments:

Powered By Blogger