Tuesday, 9 June 2009

CSKA Sofia yaishitaki Manchester United ikidai ipewe mgao wa ununuzi wa Dimitar Berbatov!!!!
• Klabu hiyo ya Bulgaria inadai Pauni Laki 4.75!!!!

• Kesi iko FIFA baada ya Man U kugoma kulipa!!
Katika hatua ya kushangaza, kustajabisha na bila kutegemewa Klabu ya Bulgaria CSKA Sofia, ambayo ndio Klabu ya kwanza kwa Dimitar Berbatov kuichezea, imefungua kesi kwa FIFA kuidai Manchester United fedha chini ya kipengele cha FIFA kinachotaka Klabu kulipwa fedha zilizobatizwa na FIFA jina la ‘mgao wa udugu’ ambao unatokana na sehemu ya malipo ya pesa za uhamisho za Mchezaji ambazo hulipwa kwa Klabu ‘iliyomwendeleza’ Mchezaji Chipukizi anaehamishwa.
Dimitar Berbatov alihamia Manchester United akitokea Tottenham Hotspurs Septemba 1 mwaka jana kwa kitita cha Pauni Milioni 30.75 na CSKA Sofia wanadai walipwe Pauni Laki 4.75 kutokana na ada hiyo.
Cha ajabu ni kuwa, Berbatov ambae ameichezea Timu ya Taifa ya Bulgaria mara 68, alihama CSKA Sofia kwenda Klabu ya Ujerumani Bayer Leverkusen mwaka 2001 na mwaka 2006 akahamia Tottenham kutoka Klabu hiyo ya Ujerumani.
Ingawa FIFA walianzisha mgao huo uliobatizwa ‘mgao wa udugu’ mwaka 2001 ili kuzilipa fidia Klabu zilizomwendeleza na kumkuza Mchezaji Chipukizi lakini kesi hii ya CSKA Sofia inashangaza sana kwa sababu Manchester United si Klabu ya kwanza kwa Dimitar Berbatov.
Manchester United imegoma kuwalipa CSKA Sofia na sasa FIFA watasikiliza shauri hili mwishoni mwa Juni.
Wenger amwinda Vermaelen!!
Kuna taarifa zenye uzito mkubwa kuwa Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, anataka kumchukua Mchezaji wa Ajax ya Uholanzi, Thomas Vermaelen, umri miaka 23, ambae ni Nahodha wa Ajax na Mchezaji wa Kimataifa wa Ubelgiji, anaecheza kama Mlinzi wa Kati, yaani Sentahafu.
Taarifa zinasema Vermaelen amepewa ofa ya mkataba wa miaka minne na mazungumzo kukamilisha dili hii yatafanyika kabla ya mwisho wa wiki hii.
Vermaelen mwenyewa amesema: ‘Kuhamia Arsenal ni njia sahihi! Kifedha ntakuwa bora na kimichezo ni ushindani mzuri kwangu!’
Rafa Benitez: ‘Vijisenti vya kununua Wachezaji vipo!’
Bosi wa Liverpool, Rafa Benitez, ili kuwapoza Mashabiki baada ya kuibuka habari kuwa Klabu imepata hasara kubwa mwaka jana na inayumba katika malipo ya deni kubwa linaloikabili, ametamka kuwa anazo pesa za kutosha za kununua Wachezaji kadhaa kwa msimu ujao.
Liverpool, inayomilikiwa na Wamarekani wawili Tom Hicks na George Gillett, imepata hasara ya Pauni Milioni 42.6 mwaka jana na inakabiliwa na utata wa jinsi ya kulilipa deni lao la Pauni Milioni 350 ambalo Klabu inalo kutokana na Wamarekani hao wawili kukopa ili kuinunua Klabu hiyo.
Benitez amesema: ‘Hali ngumu lakini dunia nzima ina matatizo haya. Ni kweli hatuna pesa nyingi kununua Wachezaji lakini tunazo za kutosha kununua mmoja au wawili.’
FA kuwarudishia pesa Washabiki watakaoshindwa kwenda Wembley kesho!!
Kutokana mgomo wa Wafanyakazi wa Treni mjini London, maarufu kwa jina la ‘Tube’, FA, Chama cha Soka England, kimeahidi kuwarudishia fedha Mashabiki wote wenye tiketi ambao watashindwa kwenda Wembley kuona pambano la kesho la Kombe la Dunia kati ya England na Andorra.
Mgomo huo wa Wafanyakazi wa Treni wa muda wa masaa 48 unaanza leo usiku na unategemewa kuwaathiri Mashabiki zaidi ya 70,000 wanaotegemewa kwenda Uwanjani Wembley.
FA imesema ilisimamisha mauzo ya tiketi wiki iliyopita ilipobainika kuna mgomo huo lakini haikufikiria kuiomba FIFA kuahirisha mechi hiyo.
England mpaka sasa ndio wanaoongoza Kundi la 6 la Nchi za Ulaya zinazogombea kuingia Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani wakiwa na pointi 18 wakifuatiwa na Croatia wenye pointi 11.

No comments:

Powered By Blogger