Sunday 25 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Man City kulizwa na sheria mpya ya Usajili Wachezaji
Sheria mpya inayoanza kutumika Msimu huu ya kutaka kila Klabu ya Ligi Kuu England isajili Wachezaji 25 na kuwasilisha majina yao ifikapo Septemba Mosi huku Wachezaji 8 kati ya hao 25 ni lazima wawe ‘wamelelewa’ kwenye Klabu za England au Wales kwa Misimu mitatu mfululizo kabla hawajatimiza Umri wa Miaka 21, huenda ikawakata maini Manchester City.
Sheria hiyo itawafanya Manchester City waathirike mno na huenda wakalazimika kuwatema hadi Wachezaji 12 kabla Dirisha la Uhamisho halijafungwa hapo Agosti 31.
Sheria hiyo mpya inaruhusu Klabu kuwa na zaidi ya Wachezaji 25 ikiwa tu hao Wachezaji wa ziada wako chini ya Miaka 21 na ‘wamelelewa’ England au Wales kwa Misimu mitatu mfululizo.
Wachunguzi wanahisi Wachezaji walio hatarini kutemwa na Man City ni kundi la kina Roque Santa Cruz, Craig Bellamy, Jo, Felipe Caicedo, Micah Richards, Michael Johnson, Vincent Kompany, Shaun Wright-Phillips, Stephen Ireland, Nigel De Jong, Kelvin Etuhu, Pablo Zabaleta na Nedum Onuoha.
Meneja wa Man City Roberto Mancini amekiri kuwepo kwa tatizo hilo: "Najua lazima tuwauze baadhi ya Wachezaji. Inabidi tuwe na listi ya Wachezaji 25.”
Hodgson akiri Torres ni kitendawili
Meneja mpya wa Liverpool, Roy Hodgson, licha ya kumtaka Straika Staa Fernando Torres abakie Liverpool kama mwenzie Steven Gerrard, ameonyesha wasiwasi kama Mhispania huyo atabaki Anfield.
Hodgson alikutana na Torres wiki iliyokwisha lakini amedokeza kuwa Nyota huyo anasita kutoa msimamo thabiti kama atabaki Liverpool.
Hodgson amesema: “Bahati mbaya sina cha zaidi cha kufanya. Torres ana bifu na Klabu na si mimi. Yeye ameniambia ana madai na Klabu ya tangu siku za nyuma hivyo mimi sina uwezo kuhusu hilo.”
Ancelotti adai Cole haendi Real
Huku kukiwa na uvumi mzito kwamba Ashley Cole yuko njiani kwenda Real Madrid kuungana tena na Jose Mourinho, Mtu ambae ndie aliemrubuni ang’oke Arsenal na kuhamia Chelsea wakati Mourinho yuko Chelsea, Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti ameonyesha imani yake kuwa Fulbeki huyo atabaki Stamford Bridge.
Ancelotti ametamka: “Cole ni Mchezaji wa Chelsea na hakuna anaetaka kumuuza. Yeye ni Mchezaji bora Duniani kwenye nafasi yake na yuko na furaha hapa. Haongoki ng’o!”
Mwalimu wa Viungo akimbizwa toka Marekani kwenda kuwanoa Rooney na Wenzake!!!
Wachezaji wa Manchester United waliocheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na kupewa likizo ndefu na kutakiwa warudi Manchester Julai 28, watakuwa chini ya Mwalimu Mkuu wa Mazoezi ya Viungo, Strudwick, ambae yupo kwenye ziara ya Man United huko Marekani na ataruka toka huko Jumapili jioni kurudi Manchester.
Wachezaji hao ni Wayne Rooney, Michael Carrick, Patrice Evra, Nemanja Vidic na Ji-sung Park.
Kocha wa Manchester United amesema hataki kuwaharakisha Wachezaji hao Mastaa kucheza hadi wawe fiti na hivyo hawatacheza mechi na Chelsea kugombea Ngao ya Hisani hapo Agosti 8.
Kocha huyo wa Viungo, Strudwick, amesema: “Kitu muhimu kwanza ni kujua wapo katika hali gani. Tutawapa programu kulingana na kiwango alicho fiti kila Mchezaji.”
Man United leo usiku wanacheza huko Kansas City, Marekani na Kasas City na baadae wataruka hadi Houston kucheza na Kombaini ya Nyota wa MLS siku ya Jumatano.

No comments:

Powered By Blogger