Wednesday 28 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com


Maradona baibai Argentina
Chama cha Soka cha Argentina, AFA, kimetamka hakitaongeza Mkataba kwa Diego Maradona kuendelea kuwa Kocha wao ingawa walitaka aendelee lakini kukawa na kutokubaliana kuhusu kuwepo kwa baadhi ya Wasaidizi wa Maradona.
Maradona alikiri kuwa yuko tayari kuendelea kama Kocha lakini hakutaka kuwabadilisha baadhi ya Wasaidizi wake ambao AFA ilikuwa haiwataki.
Rais wa AFA, Julio Grondona, ametamka: “Ili kuwa ngumu kukubaliana kuhusu kuondolewa kwa Wasaidizi wake.”
Argentina sasa itakuwa chini ya Kocha wa muda, Batista, ambae kazi yake ya kwanza itakuwa kuisimamia Nchi hiyo kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Ireland hapo Agosti 11 huko Dublin, Ireland.
El Chicharito angojewa kushangiliwa na Jamii ya Kimexico Houston!!!
Javier Hernandez, Miaka 22, leo anategemewa kucheza mechi yake ya kwanza kwa Klabu yake mpya Manchester United huko Houston, Marekani dhidi ya Kombaini ya Mastaa wa MLS, Ligi ya Marekani, Jijini Houston ambako kuna Watu wa asili ya Mexico wengi sana na wenye hamu ya kumuona Staa wao alieifungia Mexico bao 2 huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Hernandez, aka ‘El Chicharito’ yaani njegere ndogo, amejiunga na Man United kutoka Klabu ya Mexico Chivas Guadalajara.
Meneja wa Man United, Sir Alex Ferguson, amesema wataangalia kama Hernandez yuko fiti kwa vile alijiunga jana tu na Kikosi chake akitokea likizo lakini huenda akacheza kidogo kwenye mechi hiyo na Mastaa wa MLS kwa vile Wamexico wengi wanataka kumuona.
Baba Mzazi na Babu yake Hernandez walikuwa Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mexico na jina la ‘El Chicharito’ limetokana na jina la utani la Baba yake aliekuwa akiitwa ‘El Chicharo’ yaani njegere.
Wenger: “Fabregas hauzwi, Barca ni wapiga kelele tu!”
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema Arsenal haina nia ya kumuuza Nahodha wao Cesc Fabregas licha ya Barcelona kuonyesha nia ya kumtaka.
Barcelona walitoa ofa ya Pauni Milioni 29 lakini Arsenal wakaikataa na baada ya hapo Arsenal wamekataa kabisa kufanya mazungumzo na Barcelona.
Wenger amesisitiza msimamo wa Arsenal kwa kusema: “Hizo ni kelele zao, sisi hatuna nia kumuuza! Yeye ni Mchezaji muhimu kwetu na ni Kepteni wetu.”
Fabregas, Miaka23, alijiunga na Arsenal akiwa na Miaka 16 tu Mwaka 2003 akitokea Barcelona na mpaka sasa ameshaichezea Arsenal Mechi 267 na kufunga mabao 48.

No comments:

Powered By Blogger