Saturday 31 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

EMIRATES CUP: Yaanza leo!
Celtic 2 Lyon 2
Arsenal 1 AC Milan 1
Lile Kombe la Emirates ambalo huchezwa kila Mwaka Uwanja wa Emirates, nyumbani kwa Arsenal, kabla Msimu haujaanza ili kuzipa mazoezi Timu shiriki, leo limeanza kushindaniwa na Timu 4.
Katika Mechi ya kwanza Celtic ya Scotland ilitoka sare 2-2 na Lyon ya Ufaransa.
Lyon ndio walikuwa wa kwanza kupata mabao yao kupitia Michel Bastos dakika ya 28 na kwenye dakika ya 54 Harru Novillo akapachika bao la pili.
Celtic wakajitutumua na kupata bao la kwanza dakika ya 82 Mfungaji akiwa Gary Cooper na dakika ya 89 Georgios Samaras akasawazisha.
Wenyeji Arsenal walitinga kupambana na AC Milan katika Mechi ya pili na Mchezaji mpya Marouane Chamakh ndie aliefunga bao lao lakini Straika hatari wa AC Milan Alesandro Pato akasawazisha.
Kesho Jumapili Agosti 1, AC Milan v Lyon na Arsenal v Celtic.
Chicharito namba ipo Man United!
Javier Hernandez, maarufu Chicharito, ambae alijiunga Manchester United akitokea Klabu ya Mexico, Deportivo Chivas Guadalajara kabla ya Fainali za Kombe la Dunia kuanza, alidhaniwa kuwa amekwenda Old Trafford kujaza idadi tu lakini Soka lake kwenye Kombe la Dunia na kiwango chake kwenye Mechi mbili alizocheza Man United kimeonyesha atapata namba kwenye Kikosi cha Kwanza.
Hilo limeungwa mkono na Sir Alex Ferguson ambae amesema: “Amecheza na Timu pinzani ngumu na ameonyesha kiwango cha juu. Anamudu vizuri kukontroli mpira na kuumiliki na hivyo ni vitu muhimu kwenye Ligi Kuu.”
Mafowadi wanaogombea namba huko Man United ni Rooney, Berbatov, Hernandez, Michael Owen, Mame Biram Diouf, Federico Macheda na Danny Welbeck.
Lakini Welbeck yuko mbioni kujiunga na Sunderland kwa mkopo.
Mido kuikomoa Boro!
Inadaiwa Mchezaji kutoka Misri Mido amekasirishwa na Klabu yake Middlesbrough kuikataa ofa ya Pauni Milioni 2 ili ahamie Ajax huko Uholanzi waking’ang’ania walipwe zaidi.
Mido, ambae alihamia Boro 2007 akitokea Tottenham, amedaiwa kusema yuko tayari kubakia hapo Boro kwa Miezi 12 iliyobaki kwenye Mkataba wake bila kuchezeshwa na kisha aondoke kama Mchezaji huru na hivyo kuikosesha Boro ada ya uhamisho.
Mido, Miaka 27, anaelipwa Mshahara wa Pauni 40,000 kwa Wiki, amedai: “Siondoki mpaka ofa nzuri ipatikane na siondoki mpaka wanilipe bonasi zangu ninazostahili! Hii si mara ya kwanza kukataa kunilipa!”
Mido pia amekasirishwa na kitendo cha Kocha Gordon Strachan kumuacha kwenye ziara ya Ireland na Ujerumani kwa madai hayuko fiti na ikabidi abaki Klabuni afanye mazoezi zaidi.
CAS yaruhusu Wachezaji wa Northern Ireland kuchezea Republic of Ireland
CAS [Court of Arbitration for Sport], Mahakama ya Usuluhishi kwenye Michezo, imetupilia mbali Rufaa ya Chama cha Soka cha Northern Ireland iliyodai kuwa Republic of Ireland ‘ilimteka’ Fowadi Chipukizi Daniel Kearns.
Kearns, Miaka 18, alizaliwa Belfast, Northern Ireland na akaichezea Nchi hiyo kwenye michuano ya Kimataifa ya Vijana lakini akahamia kuichezea Republic of Ireland [Mji Mkuu ni Dublin] mwanzoni mwa Mwaka huu na hilo limewakera Northern Ireland na wakakata Rufaa FIFA ambao waliibwaga Rufaa hiyo na kumruhusu Kearns kuchagua Nchi ya kuchezea kwa vile amezaliwa Visiwa vya Ireland vyenye Nchi hizo mbili.
Ndipo Northern Ireland wakakata Rufaa CAS ambako nako wamebwagwa.
Ingawa Northern Ireland imesikitishwa na uamuzi huo lakini wameukubali kwa shingo upande.
Wachezaji wengi wa Northern Ireland huamua kuichezea Republic of Ireland na mfano ni Darron Gibson wa Manchester United ambae Wazazi wake walizaliwa Northern Ireland lakini yeye ameamua kuichezea Republic of Ireland.

No comments:

Powered By Blogger