Tuesday, 23 June 2009

Malouda asaini upya Chelsea!!
Winga wa Chelsea Florent Malouda amesaini mkataba mpya wa miaka minne na Klabu yake huku kukiwa kumesalia miaka miwili kwenye mkataba wa sasa.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 29 alikuwa amezungukwa na minong’ono mikubwa kwamba atauzwa hasa baada ya kuonekana anapwaya enzi za Kocha Luis Felipe Scolari.
Lakini tangu alipotua Meneja mpya wa ‘mpito’ Mdachi Guus Hiddink kuchukua nafasi ya Scolari, Malouda alizaliwa upya na kuonyesha cheche zilizomfanya acheze jumla ya mechi 31 na kufunga mabao 9 na kuiwezesha Chelsea kufika Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na kutwaa Kombe la FA.
Malouda alitua Stamford Bridge mwaka 2007 akitokea Klabu ya Lyon ya Ufaransa.
FIFA yaridhishwa na uandaaji wa Kombe la Mabara huko Bondeni
FIFA imetamka imeridhika na maandalizi na uendeshwaji wa Kombe la Mabara huko Afrika Kusini lakini imekiri bado kuna matatizo yanayobidi yamalizwe kabla ya Fainali ya Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini.
Huku kukiwa na mahudhurio mabovu ya Watazamaji, matatizo ya usafiri na uhaba wa Vyumba Mahotelini, FIFA imekiri Kombe la Mabara si Fainali za Kombe la Dunia lakini wamepata fununu kubwa nini wategemee ngoma ikilia.
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valckle, amesema: ‘Kwa sasa tumeridhika. Dunia sasa inajua Afrika Kusini wanaweza kuandaa mashindano makubwa.’
Kitu kikubwa kilichokuwa kikihofiwa ni usalama wa Mashabiki na hili lilijichomoza hasa baada ya Timu za Misri na Brazil kuibiwa vitu na pesa kwa baadhi ya Wachezaji wao toka kwenye vyumba vya Hoteli zao.
Lakini FIFA imesema imeridhishwa kwa ujumla kuhusu usalama na ushirikiano walioupata toka kwa wahusika wote.

No comments:

Powered By Blogger