Sunday 21 June 2009

Mmoja wa Wamiliki wa Liverpool kuuza mali zake kuikwamua Liverpool!!!!!!
George Gillet, mmoja wa Wamarekani wawili wanaomiliki Liverpool, yuko mbioni kuuza baadhi ya rasilimali zake ili kupunguza makali yanayoikabili Klabu ya Liverpool hasa likiwa deni la Pauni Milioni 350 ambalo linatakiwa lilipwe ifikapo Julai 24. Liverpool inamilikiwa na Wamarekani wawili mmoja akiwa huyo George Gillet na mwingine ni Tom Hicks na waliinunua Liverpool Februari 2007 na kuweka ahadi kibao kubwa ikiwa ni kujenga Uwanja mpya utakaokuwa na ujazo mkubwa lakini hadi leo ahadi hizo zote hakuna hata moja iliyotimizika na badala yake Klabu imeingia kwenye lindi la madeni.
Mbali ya deni hilo la Pauni Milioni 350 linalotakiwa kulipwa Julai 24, Wakaguzi wa Mahesabu walitangaza kuwa kwa mwaka ulioishia Agosti 2008, Klabu ilipata hasara ya Pauni Milioni 42.6 na hasara kubwa ni riba ya deni hilo kubwa.
Ili kuinusuru Klabu, George Gillet ameamua kuuza hisa zake kwenye Timu kubwa ya Mpira wa Magongo wa Barafu, Montreal Canadiens, iliyoko Canada na inategemewa atapata zaidi ya Pauni Milioni 300 kutokana na mauzo ya Uwanja wa Timu hiyo na Kampuni yake tanzu ambayo yeye anaimiliki kwa asilimia 80.
Ronaldo ajutia kuwa chanzo cha mfarakano kati ya Man U na Real!!!
Asema Ferguson ni Baba yake!!!
Anena ni heshima iliyotukuka kuvaa Jezi Namba 7 Man U!!!
Cristiano Ronaldo, ambae yuko mbioni kukamilisha uhamisho kutoka Manchester United kwenda Real Madrid utakaogharimu Pauni Milioni 80 ikiwa ni rekodi ya dunia, amesema anajuta kuwa chanzo cha mgogoro kati ya Klabu hizo mbili na wa kulaumiwa ni yeye na si Klabu hizo.
Ronaldo amesema: ‘Kulikuwa hamna makubaliano kati ya Klabu hizo. Ni mimi niliefungua mdomo na kukaribisha kila aina ya matatizo!’
Ronaldo akasisitiza juu ya heshima yake kwa Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, na kusisitiza: ‘Nimesema mara nyingi tu, yeye ni kama Baba yangu! Amenifundisha mengi sana na sijawahi kukutana na mtu mwenye moyo na munkari na soka kama yeye! Yeye ndio amenipa moto wote na kunifanya niwe mshindi! Amenifundisha ukiwa nambari mbili huna maana!’
Ronaldo anaendelea: ‘Nimepata vitu vingi toka kwake vinavyonifanya niwe mtu bora! Watu hawaelewi jinsi anavyowajali na kuwatunza Wachezaji wake hata nje ya Uwanja! Anamjali kila mmoja wa Wachezaji wake!’
Akizungumzia alivyojiunga Manchester United na kupewa Jezi Namba 7 ambayo kihistoria Klabuni hapo imevaliwa na Wachezaji mahiri kama vile George Best, Bryan Robson, Eric Cantona na David Beckham, Ronaldo ametamka: ‘Sir Alex alionyesha imani kubwa kwangu tangu nikiwa mdogo! Nilipotua Man U alinikabidhi Jezi Namba 7 na nikasita kuichukua. Akaniweka chini na kuniambia historia ya Jezi hiyo namba 7 na akaniuliza: Unaelewa nnachotaka kukuambia? Akaongeza kuwa wewe unastahili kuvaa Jezi hii!!’
Ronaldo, huku akionekana kusononeka, akatamka: ‘Nikifikiria Wachezaji Bora wa Man U waliovaa Jezi ile Namba 7, sasa naelewa jinsi alivyoniamini na kunipenda! Naomba na mimi nionekane kama wale Wachezaji Bora waliopita waliovaa Jezi ile Namba 7!!!

No comments:

Powered By Blogger