Sunday, 21 June 2009

Spain 2 Afrika Kusini 0

Afrika Kusini watinga Nusu Fainali licha ya kufungwa!!!

Wenyeji Afrika Kusini wamepigwa 2-0 na Spain lakini wametinga Nusu Fainali baada ya Iraq, katika mechi nyingine ya KUNDI A, kushindwa kuifunga New Zealand na hivyo kujikosesha nafasi ya kwenda Nusu Fainali.
Ingawa Afrika Kusini walifungwa mechi hii, walipata nafasi kadhaa walizozikosa.
Hata Kipa wao, Itumeleng Khune, alikuwa shujaa alipookoa penalti dakika ya 51 iliyopigwa na David Villa lakini, dakika moja baadae, alishindwa kuzuia mkwaju wa Villa uliotinga wavuni na kuandika bao la kwanza.
Mchezaji alieingizwa kutoka benchi, Llorente, alifunga bao la pili kwa Spain dakika ya 72.
Spain atacheza na Mshindi wa Pili KUNDI B ambao wanamaliza mechi zao leo usiku.
Iraq 0 New Zealand 0
Iraq wameikosa nafasi murua ya kusonga kuingia Nusu Fainali pale waliposhindwa kuifunga New Zealand.
Kwa Spain kuifunga Afrika Kusini, Iraq alihitaji ushindi wa aina yeyote ile ili kusonga mbele lakini walishindwa kuupata katika mechi ambayo Timu yeyote katika hizo mbili ilikuwa na uwezo wa kushinda kwa jinsi mechi ilivyokuwa wazi.
KUNDI B: Nani kutinga Nusu Fainali?
Leo Saa 3 na nusu usiku ni mechi za mwisho KUNDI B wakati Brazil, anaeongoza Kundi hili kwa pointi 6 baada ya kushinda mechi zote mbili, anapambana na Italia mwenye pointi 3.
Misri, mwenye pointi 3 pia, anacheza na USA aliekwisha kuaga mashindano haya kwa kufungwa mechi zake zote mbili.
Kimahesabu, Brazil, Italia na Misri zote zina nafasi ya kusonga Nusu Fainali ingawa ukweli ni kwamba ni Brazil tu ndie mwenye nafasi kubwa zaidi.
Italia hana ujanja ni lazima ashinde na kuomba Misri asipate ushindi mkubwa au akwamishwe na USA.
Kwa Misri nao hali ni hiyo hiyo, lazima ashinde na aombee Italia akwame.

No comments:

Powered By Blogger