Thursday 25 June 2009

NUSU FAINALI BONDENI: AFRIKA KUSINI v BRAZIL LEO!!!
Jana, Timu Bora Duniani, Spain, ilipata mkong’oto na USA bila kutarajiwa na kuaga Kombe la Mabara baada ya kipigo cha 2-0 kilichowaacha USA wakijikita Fainali kusubiri mshindi wa leo kati ya Wenyeji Afrika Kusini na Brazil mechi iitakayoanza saa 3 na nusu, saa za bongo, huko Johannesburg, Uwanja wa Ellis Park.
Timu zote, Afrika Kusini na Brazil, zitakosa Mchezaji mmoja kila upande huku Afrika Kusini kumkosa Kiungo Macbeth Sibaya ambae hachezi kwa kuwa na Kadi na Brazil watamkosa Mlinzi Juan ambae ni majeruhi.
Kwa Afrika Kusini, mbadala ni Lance Davids na Brazil ni Luisao.
Nchi hizi zimeshawahi kukutana mara mbili, mara zote zikiwa mechi za kirafiki na zote zilifanyika mjini Johannesburg na Brazil kushinda ya kwanza mabao 3-2 mwaka 1996 katika mechi ambayo Afrika Kusini waliongoza mabao 2-0 kwa magoli yaliyofungwa na Lucas Radebe na Doctor Khumalo lakini Brazil wakaibuka kidedea kwa mabao matatu yaliyofungwa na Rivaldo, Bebeto na Romario.
Mechi ya pili ilichezwa mwaka 1997, Nahodha wa Brazil kwenye mechi hiyo alikuwa Meneja wa sasa wa Brazil, Dunga, na Brazil walishinda 2-1.
Timu leo zitashuka uwanjani huku Brazil wakiwa na Jezi zao za kawaida za njano na Afrika Kusini itabidi wabadili na kuvaa za kijani.
Kocha wa Afrika Kusini, Joel Santana kutoka Brazil, anasema: ‘Tumestahili kuwa Nusu Fainali.’
Nae Dunga ametamka: ‘Afrika Kusini ni timu inayochipukia na tunajua mechi itakuwa ngumu. Wana nguvu, wepesi na mashabiki uwanja mzima ni wa kwao! Lakini tuko tayari, Brazil ni Kikosi imara na kila Mchezaji hapa anastahili kuwa timu ya kwanza!’

No comments:

Powered By Blogger