Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti amekubali kuwa Timu yake Chelsea kwa sasa ipo hoi bin taabani kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika mechi za hivi karibuni na kudorora kwao kumefuatia mara baada ya kuikung’uta Arsenal 3-0 kwenye Ligi Kuu mwezi uliopita.
Tangu ushindi huo wa kishindo Chelsea wameshinda mechi moja tu katika 5 walizocheza na sasa wapinzani wao Manchester United na Arsenal wameikaribia mno kwenye msimamo wa Ligi.
Chelsea bado wanaongoza Ligi Kuu wakiwa na pointi 42 wakifuatiwa na Man Uwenye pointi 40 na Arsenal pointi 38.
Ancelotti amekiri kupwaya kwao na amesema: “Ni kweli tumepoteza mwelekeo lakini bado tuna uwezo wa kutwaa Ubingwa! Ni mbio ndefu na sasa tuko Nusu tu!”
Leo jioni Chelsea watakuwa nyumbani Stamford Bridge kuikwaa Timu ngumu Fulham kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Rooney apona kuzivaa hasira za Fergie!!!
Wayne Rooney amepona kukumbana na hasira za Meneja wake Sir Alex Ferguson hapo jana baada ya kufanya kosa kubwa lililoisaidia Hull City kupata bao la kusawazisha kwenye mechi ya Ligi Kuu ambayo hatimaye Manchester United walishinda mabao 3-1.
Rooney ndie aliewafungia Man U bao la kwanza dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili Rooney alifanya kosa kubwa pale pasi yake aliyotaka kumrudishia Kipa wake Kuszczak kunaswa na Craig Fagan aliemtilia pasi mwenzake Altidore lakini aliangushwa na Beki wa Man U Rafael kwenye boksi na ndipo Fagan akasawazisha kwa penalti.
Rooney amesema: “Goli lao la kusawazisha ni kosa langu! Meneja wangu asingefurahishwa lakini bahati tumeshinda!”
Baada ya kosa lake, Rooney alicheza kufa na kupona na kusababisha bao la pili pale krosi yake ilipombabaisha Beki wa Hull Andy Dawson na kujifunga mwenyewe.
Kisha Rooney akatengeneza bao la 3 na kumpa pasi Berbatov aliepachika bao hilo.
Ferguson alimsifia Rooney kwa kusema: “Ni mpiganaji! Alifanya kosa moja lakini yeye ni mshindi! Alijisahihisha na kuutengeneza ushindi wetu!”Kwa goli lake la jana sasa Rooney ana magoli 13 kwenye Ligi Kuu na amefungana na Defoe pamoja na Drogba katika Ufungaji goli nyingi.
No comments:
Post a Comment