Friday 1 January 2010

Wachezaji Pompey waingiwa hofu kuhusu Mishahara yao!!!
Mlinzi wa Portsmouth Steve Finnan ametoboa kuwa Wachezaji wa Timu hiyo wameingiwa na hofu kubwa kuhusu hali ya kifedha ya Klabu hiyo ambayo, kwa mara ya 3 sasa, wameshindwa kulipa Mishahara kwa wakati na safari hii wameahidiwa kulipwa siku ya Jumanne mara baada ya Sikukuu ya Mwaka mpya.
Portsmouth, ambao wako mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pia wametakiwa kufilisiwa na Mamlaka ya Kodi ya Mapato kwa kuwa wana deni la kodi la Pauni Milioni 60.
Finnan amesema: “Wachezaji wana wasiwasi na si jambo zuri kwa Mashabiki!! Tuliwasikia juzi kwenye mechi na Arsenal wakiimba kulalamikia hali yetu!!”
Kesho Portsmouth wanacheza na Coventry kwenye Mtoano wa Raundi ya Tatu ya Kombe la FA na Finnan amewaahidi Washabiki kuwa wakiingia uwanjani matatizo yao yote watayaweka kando na kucheza kufa kupona.
McCarthy: Wakati wa kuondoka umefika!!!
Benni McCarthy, miaka 32, kutoka Afrika Kusini anaechezea Klabu ya Blackburn Rovers amekiri kuwa sasa umefika wakati wa yeye kutafuta Timu nyingine ili apate namba ya kudumu ili aweze kuchaguliwa kwenye Kikosi cha Bafana Bafana kitakachokuwa Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia mwezi Juni.
McCarthy ameanza mechi 6 tu Msimu huu wa Ligi hapo Blackburn.
McCarthy amesema: “Ningependa kubaki England, ni Ligi bora! Sina furaha na hali ya sasa, nataka nicheze kila mara ili nichukuliwe Bafana Bafana!”
McCarthy alijiunga na Blackburn mwaka 2006 akitokea FC Porto ya Ureno na amefunga goli 52 katika mechi 136 alizoichezea Blackburn.
Song aimba: Hakuna mtu anaweza kuifunga Arsenal!!!!
Kiungo kutoka Cameroun Alex Song anaechezea Arsenal ametamba kuwa hakuna Timu inayoweza kuifunga Arsenal.
Arsenal wako pointi 4 nyuma ya vinara wa Ligi Chelsea lakini wana mechi moja mkononi na wataicheza mechi hiyo Jumatano ijayo kwa kupambana na Bolton Wanderers.
Song ametamba: “Tukicheza kama tulivyoifunga Portsmouth 4-1 hapo juzi, hakuna mtu anaeweza kutufunga!!”
Portsmouth ndio Timu iliyo ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Song anategemewa kesho kucheza katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya West Ham na kisha kusafiri ili kujiunga na Timu ya Taifa ya Cameroun inayojitayarisha kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazoanza Januari 10 huko Angola.

No comments:

Powered By Blogger