Saturday 2 January 2010

KOMBE LA FA: Man Utd v Leeds inakumbusha uhasama wa enzi!!!
Kihistoria Manchester United ikipambana na Leeds United ni mechi ya uhasama kwa Wachezaji wa pande hizo mbili pamoja na Mashabiki wa Timu hizo zinazotoka Miji ya Manchester na Leeds inayotenganishwa na Maili 40 tu.
Chimbuko la uhasama huo ni Vita ya Mawaridi iliyopiganwa Karne ya 15 lakini kimpira uhasama huu ulikuzwa miaka ya 1970 wakati Leeds United walikuwa na Genge la Mashabiki waliojiita Kruu wa Kazi [Service Crew] na Manchester United Genge lao liliitwa Jeshi Jekundu [Red Army].
Kwa miaka ya hivi karibuni uhasama huu umepungua kwa vile Leeds United wameporomoka kutoka Lig Kuu toka mwaka 2004waliposhushwa Daraja na Timu hizi hazijakutana tangu wakati huo.
Kwa sasa Leeds United wako Daraja la Ligi 1 ambalo ni Madaraja mawili chini ya Ligi Kuu, yaani baada ya Ligi Kuu lipo Daraja la Championship na kisha Ligi 1.
Leeds United kwa sasa ndio wanaoongoza msimamo wa Ligi 1.
Lakini kesho, saa 10 jioni saa za bongo, Leeds United watatua Old Trafford kuvaana na Manchester United kwenye Raundi ya 3 ya Kombe la FA, na uhasama unategemewa kuchomoza tena.
Kwa tahadhari, Polisi wa Jijini Manchester wameshawaomba Wamiliki wa Baa na Grosari kupunguza uuzaji wa pombe kabla ya mechi hiyo na pia kutowauzia pombe watu wanaoonekana tayari wako nyingi.
Pia Polisi imetoa onyo kuwa hakuna Shabiki atakaeruhusiwa kuingia Uwanjani ikiwa kalewa na mbali ya kuzuiwa upo uwezekano wa kupelekwa lupango.
Nae Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, amewatahadharisha Wachezaji wake kuepuka vitendo vinavyoweza kuchochea vurugu.
Ferguson ametamka: “Haina haja ya kukumbushia nini maana ya mechi na Leeds! Mechi hizo zimekuwa na uhasama wa kihistoria na ni lazima Wachezaji wa pande zote mbili wajichunge ili wasilipue vurugu! Leeds wanaleta Mashabiki wao 8,000 Old Trafford na itakuwa ni siku ya kazi ya ziada kwa Polisi!”
Ferguson alikumbushia uhasama uliokuwepo na kukumbusha jinsi alivyotaka kushambuliwa na Mashabiki wa Leeds wakati akitoka kutazama mechi Uwanja wa Leeds uitwao Elland Road na akiwa kwenye gari lake, wakati amesimama kwenye taa nyekundu, kundi la Mashabiki wa Leeds walimtambua na kupiga kelele: “Ferguson!’ na kuanza kumkimbilia lakini, bahati nzuri, sekunde hiyo hiyo, taa zikageuka njano, na yeye akapiga msele na kutoka nduki!

No comments:

Powered By Blogger