Friday 1 January 2010

KWA WADAU WOTE:
TUNAWATAKIA KILA LA KHERI, FANAKA NA KILA KITU KWA MWAKA 2010!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!
MUNGU AWABARIKI!
Amina.
===stormingfohadi
Ancelotti ambatiza Wenger “Mchawi mzuri”!!
Carlo Ancelotti amejibu mapigo kwa Arsene Wenger, ambae hapo juzi alidai Chelsea itaanguka kadri Msimu wa Ligi unavyoendelea, kwa kumbatiza “Mchawi mzuri”!
Uongozi wa Chelsea kwenye Ligi kuu mwezi Desemba ulipunguzwa kwa pointi 9 huku Arsenal wakishinda mechi 3 mfululizo, na, baada ya kuifunga Portsmouth 4-1 huko Fratton Park siku ya Jumatano, Arsene Wenger alitangaza kuwa Chelsea watapoteza pointi na kuporomoka chini kadri Msimu unavyoendelea na pia Ancelotti atatimuliwa Chelsea ifikapo mwishoni mwa Msimu.
Ancelotti aliicheka kauli ya Wenger na kutamka: “Kama alisema hayo basi yeye ni ‘mchawi mzuri”!”
Ancelotti akaongeza: “Tulikuwa na matatizo mwezi Desemba na hatukushinda na tulitoka sare na Everton, Birmingham na West Ham lakini hilo ni kawaida! Kila Timu ina kipindi chake kigumu!”
Hata hivyo, mpaka sasa mwaka 2010 ukianza, Chelsea ndio wanaongoza Ligi wakiwa na pointi 45, Manchester United ni wa pili na wana pointi 43 na Arsenal ni wa 3 wakiwa na pointi 41 huku wamecheza mechi moja pungufu.
Jumatano ijayo Arsenal watacheza na Bolton ikiwa ndio mechi yao pungufu.
Wakati huohuo, Meneja huyo wa Chelsea amesema hatishiki na uvumi mkubwa kuwa Meneja wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho, atarudishwa tena Chelsea kuchukua nafasi yake na Ancelotti amesema: “Itabidi asubiri kwani mie ndie Meneja wa Chelsea na ntabaki hapa! Yeye ni Meneja wa Inter Milan hivyo si mpinzani wangu!”
Baada ya kipigo cha 4-1, Pompey hawana Mishahara!!!
Mara baada ya kutandikwa bao 4-1 na Arsenal kwenye Ligi Kuu Uwanjani kwao Fratton Park mbele ya Mashabiki wao waliokuwa wakiimba ‘Fukuza Bodi” na “Pesa zetu ziko wapi?’, sasa Wachezaji wa Portsmouth watakosa Mishahara yao ya Desemba hii ikiwa ni mara ya 3 kwa Timu hiyo kukosa kulipwa Mishahara yao kwa wakati.
Portsmouth pia wameshindiliwa msumari wa moto pale Mamlaka ya Kodi ya Mapato kutaka Klabu hiyo ifilisiwe kwa kushindwa kulipa Kodi inayokadiriwa kuwa ni Pauni Milioni 60.
Portsmouth pia imefungiwa na FA kutosajili Mchezaji yeyote hadi itakapolipa madeni ya kutokukamilisha malipo ya ununuzi wa Wachezaji.
Portsmouth ndio Klabu ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu na hivi karibuni ilimtimua Meneja wake na kumteua Avram Grant kushika nafasi hiyo.
Klabu ya Portsmouth imetoa taarifa kuwapoza Wadau wake kuwa itawalipa Wachezaji na Wafanyakazi wake ifikapo Januari 5 na uchelewesho huo umetokana tu na matatizo ya kiutawala na sio fedha.
Pia, wamesisitiza kuwa Mmiliki wa Klabu hiyo, Ali al-Faraj kutoka Saudi Arabia, sasa anaandaa mfumo mpya wa utawala wa kifedha ili kufuta matatizo ya uendeshaji.

No comments:

Powered By Blogger