Sunday, 31 January 2010

Adebayor: “Hayatou ameisaliti Togo!!”
Nahodha wa Togo, Emmanuel Adebayor, ambae pia huichezea Manchester City, amechukizwa na uamuzi wa CAF, Chama cha Soka cha Afrika, wa kuifungia Togo kutocheza Mashindano yajayo mawili ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kosa la kujitoa kucheza Fainali za Kombe hilo huko Angola.
Togo walijitoa baada ya Serikali yao kuwataka warudi nyumbani baada ya Dereva wa Basi lao pamoja na Kocha Msaidizi na Afisa Habari kuuawa kwa risasi wakati wakisafiri ndani ya Basi hilo kuelekea Mji wa Cabinda wakitokea Congo.
Adebayor amesema Issa Hayatou, Rais wa CAF anaetoka Cameroun, amewasaliti na inabidi aachie ngazi cheo hicho.
CAF wamedai kufungiwa kwa Togo ni kwa sababu mambo ya Soka kuingiliwa na Serikali yao.
Lakini Adebayor anadai: “Hawajali vilio vya dunia! Ni Nchi iliyotutuma twende Angola! Ni Nchi iliyotutaka turudi nyumbani kuomboleza!”
KASHFA YA TERRY: Terry kubaki Kepteni Chelsea!!
• Jana alicheza na kufunga bao la ushindi!!!
Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti amesema Beki wao John Terry atabaki kuwa Kepteni wa Klabu hiyo licha ya kulipuliwa kwa kashfa juu yake kuwa alitembea na gelfrendi wa Mchezaji mwenzake wa Chelsea wakati huo, Wayne Bridge, kashfa ambayo imeibuka na Terry kutajwa baada ya Mahakama kufutilia mbali amri ya kutomtaja Terry.
Kumekuwa na kauli mbiu kuwa Terry ambae pia ni Nahodha wa Timu ya Taifa ya England aondolewe Unahodha wa Timu hiyo ya Taifa.
Jana Chelsea waliifunga Burnsley 2-1 kwenye Ligi Kuu na Terry alicheza huku akivaa utepe wa Unahodha wa Chelsea na pia kuifungia Chelsea bao la pili na la ushindi.
Ancelotti ametamka: “Hamna mjadala kuhusu Terry. Sijui kwa nini naulizwa! Yeye ni Nahodha wetu! Klabu yote tunamsapoti yeye na familia yake!”
Mpaka sasa FA, Chama cha Soka cha England, hakijatoa tamko lolote.
Lakini Wayne Bridge, ambae kwa sasa ni Mchezaji wa Manchester City na pia huchezea England, ametoa tamko kupitia kwa Wanasheria wake wa kuomba faragha yake na familia yake iheshimiwe na asiingliwe. 

No comments:

Powered By Blogger