Thursday, 4 February 2010

Hargreaves nje UEFA!!
Owen Hargreaves hayumo kwenye Kikosi cha Wachezaji 25 cha Manchester United kilichosajiliwa UEFA ili kucheza hatua ya Mtoano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ambayo Man United watacheza na AC Milan kwenye Raundi ya Mtoano ya Timu 16 na mshindi anaingia Robo Fainali.
Hargreaves, miaka 29, hajaonekana uwanjani tangu tarehe 21 Septemba 2008 na baada ya hapo alifanyiwa operesheni ya magoti yake yote mawili yaliyokuwa yakimpa maumivu.
Ilitegemewa, na hili lilizungumzwa na Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson, kwamba Hargreaves atakuwemo kwenye Kikosi hicho cha UEFA lakini sasa nafasi yake imechukuliwa na Beki Chipukizi kutoka Ubelgiji Ritchie de Laet, miaka 21.
Ferguson alitoa matumaini hivi karibuni pale aliposema Hargreaves yupo kwenye programu ya mazoezi ya nguvu akizunguka na kupokezana kwenye Timu za Akiba na za Kwanza ya siku mbili mfululizo mazoezi na siku moja mapumziko.
Lakini inaelekea nafuu yake na kuwa fiti kumechelewa.
Katika Kikosi hicho cha Wachezaji 25, jina la Straika kijana Danny Welbeck limeondolewa kwa vile sasa yupo Preston kwa mkopo, Timu ambayo Meneja wake ni Darren Ferguson ambae ni mtoto wa Sir Alex Ferguson.
Nafasi ya Welbeck imechukuliwa na Kijana kutoka Senegal Mame Biram Diouf.
Evra: Fergie haondoki!!!
Beki wa Manchester United Patrice Evra ana imani kubwa kwamba Meneja wake Sir Alex Ferguson atabaki hapo kwa muda mrefu bila kustaafu.
Ferguson yuko kwenye wadhifa huo wa Umeneja kwa miaka 23 sasa na hajatamka lolote kuhusu lini atastaafu ingawa huko nyuma aliwahi kusema atastaafu mwishoni mwa msimu wa mwaka 2001/2 lakini akabadili uamuzi wake.
Evra alitoboa kuwa mara baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling ambayo Manchester United waliwafunga Mahasimu wao wakubwa Manchester City mabao 3-1 Uwanjani Old Trafford na kutinga Fainali, Sir Alex Ferguson alikuwa akicheza dansi kwa furaha kwenye vyumba vya kubadilishia jezi na hilo lilimdhihirishia Evra kuwa bado Ferguson ana njaa kubwa ya ushindi.
Evra amesema: “Tulimwona akirukaruka kama mtoto! Unaweza ukasema ni kama vile hajawahi kushinda mechi! Hilo linamfanya ashindwe kustaafu! Atabaki hapa hadi mwisho!”

No comments:

Powered By Blogger