Straika wa Manchester United Wayne Rooney ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Januari na David Moyes wa Everton ameipata kwa upande wa Mameneja.
Rooney kwa mwezi Januari ameifungia Man United mabao 6 na sasa ndie anaeongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 20.
Hii ni mara yake ya 5 kushinda Tuzo hii.
Meneja wa Everton, David Moyes, amepewa Tuzo ya Meneja Bora kwa Januari baada ya kuiongoza Timu yake kupata ushindi mara 3 na sare moja.
Hii ni mara yake ya 6 kuipata Tuzo hii.
Tuzo hii ya Ubora wa kila mwezi hutolewa na Barclays ambao ndio Wadhamini Wakuu wa Ligi Kuu na uchaguzi wa nani bora hufanywa na Jopo lenye Wawakilishi kutoka FA, Vyombo vya Habari, Mashabiki na Wadau mbalimbali.
Wenger ageuka Sungura Mjanja!!!
• Adai kumaliza Ligi nafasi ya 3 ni bora kuliko kubeba FA au Carling Cup!!!
Meneja wa Arsenal, Arsène Wenger, amedai kumaliza Ligi Kuu ukiwa nafasi ya 3 ni kitu bora zaidi kuliko kunyakua Makombe ya FA na Carling.
Wenger ametamka: “Ukishinda Carling Cup kwangu huniambii umeshinda kitu! Kufanya vizuri kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE ni muhimu kuliko kuchukua Carling au FA! Sisi kwa mara ya 10 mfululizo tumefuzu kuingia hatua ya Mtoano ya UEFA!”Kwa mara ya mwisho Arsenal ilitwaa taji lolote ni mwaka 2005 pale iliponyakua Kombe la FA na tangu wakati huo haijaambua kitu.
Msimu huu, Arsenal imeshatupwa nje ya Makombe ya FA na Carling na kwenye Ligi Kuu ipo nafasi ya 3 nyuma ya Chelsea na Manchester United lakini bado imo kwenye kinyang’anyiro cha UEFA CHAMPIONS LEAGUE na itacheza na FC Porto kwenye mechi za mtoano baadae mwezi huu.
Wenger alipoulizwa swali kama kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya 3 ni bora kuliko kuchukua Vikombe vya FA na Carling, alijibu: “Tupo hapa kushinda Vikombe lakini inategemea ni Vikombe vipi. Ni Ubingwa wa Ulaya, Ligi Kuu, Carling au FA? Sisi tumeingia hatua ya Mtoano ya UEFA mara 10 mfululizo na hilo ni gumu kuliko kuchukua Vikombe vya FA na Carling!”
Kuhusu kumaliza nafasi ya 3 kwenye Ligi, Wenger amesema hata hilo ni mafanikio makubwa kwani utakuwa umezipiku Timu ngumu kama Manchester City, Liverpool, Tottenham na Aston Villa.
Matamshi hayo ya Wenger yatawastua Wadau wengi wa Arsenal ambao wamebaki kwa muda mrefu sasa bila Kikombe chochote na wale wrevu watamwona sasa wenger amegeuka Sungura aliekosa kuzitungua Zabibu mbivu na badala yake kuziita mbichi.
Hata hivyo, mwenyewe Wenger hajakata tamaa kuhusu Ligi Kuu na kama vile alivyoichukulia mechi na Manchester United Jumapili iliyokwisha, mechi ya kesho na Chelsea ambayo imebatizwa Bigi Mechi, yeye haioni kama ndio itaamua kitu kwenye Ligi Kuu.
Wenger anaelezea: “Baada ya kucheza na Man United na Chelsea, hatuchezi tena nao! Kuwa nyuma yao pointi 6 sio maafa! Tulikuwa pointi 11 nyuma ya Chelsea mwishoni mwa November, kwa nini tukate tamaa tukiwa nyuma pointi 9 kesho?”
KOMBE LA DUNIA: Marefa 30 wateuliwa kwa Fainali!!
• Refa wa ‘Mkono wa Thierry Henry’ yumo!!!
Marefa 30 kutoka kila pembe ya Dunia wameteuliwa na FIFA ili kuwa waamuzi kwenye Fainalli za Kombe la Dunia zitakazochezwa Afrika ya Kuni kuanzia Juni 11 hadi Julai 11.
Mabara ambayo wanatoka Marefa hao 30 ni 10 kutoka Ulaya, 6 kutoka Marekani ya Kusini. Afrika, Asia na Nchi za Carribean, Marekani ya Kati na Kaskazini zimetoa Marefa wanne kila mmoja. New Zealand imetoa Marefa wawili.
Kila Refa atakuwa na Wasaidizi wake, yaani Washika Vibendera, ambao wamekuwa wakifanya nae kazi kwa ukaribu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kwa Nchi zilizoendelea ni wenzake toka Nchi moja.
Katika Marefa hao 30, Refa kutoka Ligi Kuu England ni Howard Webb akisaidiwa na Darren Cann na Michael Mullarkey.
Refa kutoka Sweden, Martin Hansson, alieleta mzozo mkubwa kwenye mechi ya marudiano ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Ufaransa na Ireland aliposhindwa kumuona Thierry Henry wa Ufaransa akiukontroli mpira kwa mkono na kumpasia mwenzake Gallas alieisawazishia Ufaransa na kuwa bao 1-1 katika muda wa nyongeza na hivyo kuipeleka Ufaransa Fainali Kombe la Dunia, yumo kwenye listi hiyo ya Marefa 30.
Marefa kutoka Afrika ni Mohammed Benouza kutoka Algeria, Koman Coulibaly kutoka Mali, Jerome Damon kutoka Afrika Kusini na Eddy Allen Maillet kutoka Seychelles.
No comments:
Post a Comment