Tuesday, 2 February 2010

UHAMISHO SIKU YA MWISHO: Mkenya akosa ulaji Man City!!!
• Mido, McCarthy watua West Ham!!
McDonald Mariga, miaka 22, anaechezea Klabu ya Italia Parma ambae ni Mchezaji wa Kimataifa kutoka Kenya amekataliwa kupewa kibali cha kazi cha England na hivyo kumkosesha uhamisho wa ada ya Pauni Milioni 7 kwenda Manchester City na pia kumkosesha kuwa Mchezaji wa kwanza toka Kenya kucheza Ligi Kuu England.
Mariga, aliechezea Harambee Stars mechi 24 na hivyo kutimiza kipengele kinachotaka Wachezaji kucheza asilimia 75 ya mechi za Kimataifa katika miaka miwili, ombi lake la kibali lilitupwa nje kwa vile Kenya ipo nafasi ya 98 kwenye msimamo wa ubora wa FIFA na ni Wachezaji waliotoka Nchi zilizo nafasi 70 za juu ndio wanahusishwa kupatiwa vibali.
Wakati huohuo huku ule muda wa kufungwa dirisha la uhamisho ukikaribia, Klabu kadhaa zimefanikiwa kunyakua Wachezaji katika dakika za mwisho na West Ham wameweza kuwachukua Wachezaji wawili wanaotoka Afrika.
Mido, ambae anachezea Zamalek ya Misri, amechukuliwa West Ham kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu.
Nae Benni McCarthy kutoka Afrika Kusini aliekuwa akicheza Blackburn Rovers amehamia rasmi West Ham.
Robbie Keane wa Tottenham yuko mbioni kupelekwa kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu huko Celtic ya Scotland.
Manchester City imemsaini Mchezaji kutoka Middlesbrough aitwae Adam Johnson.
Habari kamili za uhamisho tutawaletea baadae.
KASHFA YA TERRY: Wachezaji Man City wamsapoti mwenzao Bridge!!
Wacheza watatu wa Manchester City walivaa tisheti chini ya Jezi zao zilizoandikwa ‘Team Bridge’ ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono mwenzao Wayne Bridge ambae imedaiwa gelfrendi wake alitembea na Nahodha wa Chelsea na England, John Terry.
Wachezaji hao watatu walivaa tisheti hizo katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa City of Manchester Stadium Jumapili na Man City kuifunga Portsmouth 2-0.
Wachezaji hao ni Carlos Tevez, Stephen Ireland na Nigel de Jong.
Meneja wa Man City Roberto Mancini alitamka: “Wachezaji wako karibu na Wayne Bridge. Ni ishara yao kumuunga mkono.”
Mancini aliongeza: “Bridge ni Mchezaji mzuri na mtu safi sana!”
KISAGO CHA EMIRATES:
Wenger alaumu Wachezaji wake
• Fergie asifia Timu yake, Nani apewa heko!!
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amewaponda Wachezaji wake kufuatia kipigo cha 3-1 walichokipata nyumbani Uwanjani Emirates toka kwa Manchester United katika mechi ya Ligi Kuu hapo Jumapili.
Wenger alisema: “Tulikuwa wazembe! Hatukucheza kitimu! Hatukuwa kwenye fomu!”
Kipigo hicho kilimaliza wimbi la mechi 10 katika Ligi bila kufungwa baada ya kupigwa bao 3 na Chelsea Uwanjani hapo hapo Emirates mwezi Novemba mwaka jana.
Sasa Arsenal ina kibarua kingine kigumu Jumapili ijayo huko Stamford Bridge watakapoenda kuwatembelea vinara wa Ligi Chelsea.
Wenger alikiri: “Man United walikuwa bora kupita sisi! Tuliwapa nafasi kubwa! Hatukucheza vizuri na sijui kwa nini! Itabidi tubadilike kwa mechi ijayo!”
Nae Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, ameitaka Timu yake sasa ikaze buti na iendeleze wimbi la ushindi.
Ferguson amewasifia Wayne Rooney na Nani kwa uchezaji wao wa kujituma kwenye mechi hiyo.
Ferguson alisema: “Tulicheza vizuri mno! Wachezaji wote walikuwa tayari kwa pambano hili! Walikuwa shapu na walipasiana vizuri na tulipata nafasi nyingi sana za wazi!”
Ferguson aliongeza kwa kusema Timu yake hutumia sana mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza, yaani ‘kaunta ataki’, na kwa vile Arsenal wanamiliki sana mipira na huja kwenye boksi lako mara kwa mara ukiunasa mpira hapo na kushambulia kwa haraka sana utawafunga tu.
Kuhusu Rooney, Ferguson alisema: “Ana furaha hapa. Yeye hajabadilika na utajiri na ustaa haujambadilisha chochote! Watu wengi hubadilika wakifanikiwa lakini Rooney yu vilevile! Kwa mara nyingine alikuwa shujaa wetu!”
Rooney alifunga bao moja katika ushindi huo wa 3-1 dhidi ya Arsenal na hilo ni goli lake la 100 katika Ligi Kuu na limemfanya awe Mchezaji wa 18 kufunga goli 100 katika Ligi Kuu.
Kuhusu Nani, Ferguson alitamka: “Alikuwa majeruhi lakini amepona na sasa amekomaa!! Mechi zake 3 za mwisho amecheza vizuri na hii amecheza bora zaidi!”

No comments:

Powered By Blogger