Thursday 4 February 2010

Pompey yapigwa bei mara ya 4 katika mwaka mmoja!!!
Portsmouth, Klabu ya Ligi Kuu England iliyo mashakani sana ikiwa mkiani kwenye Ligi hiyo na pia kuwa taabani kifedha, imeuzwa kwa mara ya 4 katika kipindi cha mwaka mmoja na safari hii imenunuliwa na Mfanya biashara wa Hong Kong Balram Chainrai.
Wamiliki wa Klabu hiyo wa mwanzoni ni Sacha Gaydamak, Sulaiman al-Fahim na Ali al-Faraj.
Chainrai ambae alikuwa ni Mwanahisa katika Klabu hiyo iliponunuliwa na Mmiliki wa mwisho Ali al-Faraj imebidi aichukue Klabu hiyo baada ya kushindwa kumlipa pesa alizoikopesha mwanzoni mwa msimu huu.
Chainrai aliikopesha Portsmouth Pauni Milioni 17 na dhamana ilikuwa ni Uwanja wa Klabu hiyo, Fratton Park, mapato kutoka Kampuni za TV na Hisa za al-Faraj.
Portsmouth hapo jana usiku ilifungwa bao 1-0 na Fulham kwenye mechi ya Ligi Kuu na Wachezaji wao walicheza mechi hiyo huku Mishahara yao imecheleweshwa kulipwa hii ikiwa ni mara ya 4 kwa tukio kama hilo.
Vilevile, Klabu hiyo tarehe 10 Februari inatakiwa Mahakamani ilikopelekwa kufilisiwa na Mamlaka za Mapato ya Kodi kwa kushindwa kulipa kodi.
Portsmouth pia imefungiwa kusajili Mchezaji yeyote kwa kushindwa kulipa madeni kwa Klabu nyingine yanayotokana na ununuzi wa Wachezaji na hili limesababisha FA kuchukua pesa zao za mapato toka Kampuni za TV ili kuzilipa Klabu zinazoidai.
Jumamosi, Portsmouth itakuwa Old Trafford kuchuana na Mabingwa Manchester United kwenye mechi ya Ligi Kuu.

No comments:

Powered By Blogger