Wednesday 3 February 2010

FA CUP: Crystal Palace na Notts County wazinanga Timu Kubwa!!!
• Mufilisi Palace wairarua Wolves!!
• County waipiga Wigan!!
Crystal Palace na Notts County, Klabu za Daraja la chini, zimezitoa toka kwenye Kombe la FA Timu za Ligi Kuu Wolves na Wigan katika mechi za marudiano hapo jana baada ya kutoka suluhu mechi za awali.
Crystal Palace ambayo iko hali mbaya kifedha na huenda ikafilisiwa imeikung'uta Wolves mabao 3-1.
Notts County wao wamewapiga Wigan bao 2-0.
Crystal Palace sasa watakutana na Aston Villa kwenye Raundi ya 5 ya Kombe hilo la FA hapo Februari 14 na Notts County watacheza na Fulham.
Ancelotti amruhusu John Terry kupumzika!!
Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti amesema Nahodha wao John Terry ambae anasakamwa na skandali la kutembea na gelfrendi wa Wayne Bridge ambae alikuwa Mchezaji wa Chelsea kabla hajahamia Manchester City, yuko huru kuchukua likizo wakati wowote ili kupumzisha akili kufuatia kuandamwa kwa siku kadhaa sasa baada ya Mahakama kufuta amri ya kutomtaja jina kwenye kashfa hiyo.
Pia, kumekuwa na wito kutoka kila pembe kwa Terry kujiuzulu wadhifa wa Unahodha wa Timu ya Taifa ya England.
Tangu kuibuka kwa kashfa hiyo John Terry ameshacheza mechi mbili za Ligi Kuu ya kwanza ikiwa ile Chelsea waliyoifunga Burnley 2-1 huku Terry akifunga bao la pili na la ushindi na mechi nyingine ni ya jana Chelsea waliyotoka sare 1-1 na Hull City.
Ancelotti alitamka: “Bado anacheza vizuri! Nitamruhusu akitaka kupumzika!”
Mameneja watwangana Uwanjani!!!
Meneja wa Nottingham Forest, Billy Davies, amedai kuwa Meneja wa Derby County, Nigel Clough, alimshindilia na goti wakati kulipotokea fujo kati ya Timu hizo mbili zilipocheza wiki iliyopita na ameitaka FA imchukulie hatua kali Nigel Clough.
Hata hivyo FA imeamua kutowashitaki watu binafsi na badala yake imezishitaki Timu zote mbili kwa kuleta fujo.
Nae Nigel Clough ambae enzi za Uchezaji wake alikuwa Mchezaji wa Nottingham Forest wakati huo Baba yake Mzazi, Brian Clough, akiwa Meneja hapo Forest, amezikana tuhuma hizo za Billy Davies na kudai kuwa ikiwa alimgusa Davies basi ilikuwa ni bahati mbaya tu kwani kulikuwa na vurugu na rabsha iliyowahusu Wachezaji wa pande hizo mbili na watu wengi wengine.
Timu za Nottingham Forest na Derby County zinatoka Mji mmoja wa Derby na zilipokutana mara ya mwisho mwezi Agosti mwaka jana pia kulizuka fujo na Klabu hizo mbili zikapigwa faini na FA.

No comments:

Powered By Blogger