Friday, 5 February 2010

Terry avuliwa Unahodha England!!
John Terry amevuliwa Unahodha wa Timu ya Taifa ya England kufuatia kufumuka kwa skandali kuwa alitembea na gelfrendi wa Mchezaji mwenzake wa Chelsea wakati huo na England, Wayne Bridge.
Terry, miaka 29, leo alikuwa na mazungumzo na Meneja wa England Fabio Capello kuhusu kashfa hiyo.
Taarifa ya Capello iliyosambazwa imesema kuwa baada ya kutafakari kwa undani ni bora kumvua Unahodha Terry.
Mwenyewe Terry amesema kuwa anauheshimu uamuzi wa Capello na yuko tayari siku zote kujitolea kwa moyo wote kuisaidia Timu ya England.
Taarifa hiyo ya Capello haikutaja nani atachukua wadhifa huo ingawa iligusia kuwa Terry alipochaguliwa Nahodha pia aliteuliwa Makamu Nahodha ambae ni Rio Ferdinand na uamuzi huo haubadiliki.
Terry, mwenye umri wa miaka 29, aliteuliwa kuwa Nahodha mwaka 2008 na kulikuwa na kila dalili yeye ndie ataiongoza England kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwezi Juni.
Terry, ambae ana Mke na watoto, alitajwa kwenye Magazeti wiki iliyokwisha mara baada ya amri ya Mahakama ya kutotaja jina kufutwa na vikatoka vilio toka kila upande kwamba hafai tena kuwa Nahodha wa Timu ya Taifa ya England.
Klabu yake Terry, Chelsea, imetamka kuwa inamsapoti yeye na familia yake na imesema iko tayari kumpa likizo wakati wowote ule akiihitaji ili apunguze presha.
Ferguson aitetea rufaa ya Ferdinand
Katika rufaa ya Rio Ferdinand anayopinga kuongezewa adhabu ya kufungiwa mechi moja zaidi baada ya rufaa yake ya kupinga kufungiwa mechi 3 za awali kutupwa na Jopo la Nidhamu kwa misingi kuwa ilikuwa haina uzito na hivyo kumwongezea kifungo kwa mechi moja zaidi na kuwa jumla mechi 4, Klabu yake Manchester United itamtetea kwa kutoa mfano wa Mchezaji wa Liverpool Javier Mascherano.
Man United inadai Mascherano hakushitakiwa kwa kosa sawasawa na la Ferdinand la kumpiga Jermaine Beckford wa Leeds katika mechi iliyochezwa Septemba bila Refa Alan Wiley kuona lakini Refa huyo alipoonyeshwa video ya tendo hilo alisema asingetoa Kadi Nyekundu.
Bodi ya Rufaa itakaa Februari 12 kujadili rufaa hiyo ya pili ya Ferdinand.
Mpaka sasa Ferdinand ameshaanza kuitumikia adhabu yake na ameshaikosa mechi moja ile ya Ligi Kuu dhidi ya Arsenal na Jumamosi ataikosa nyingine ya Portsmouth ikifuatiwa na ya Aston Villa na mechi ya 4 ambayo inapingwa na Manchester United ni ile na Everton.
Lakini endapo rufaa hii ya pili ya Ferdinand itashindwa basi kuna hatari, kufuatia kanuni zilivyo, kuwa huenda akaongezewa tena adhabu ya kufungiwa mechi moja zaidi kwa kukata rufaa bila misingi na hilo likitokea basi Ferdinand ataikosa Fainali ya Kombe la Carling itakayochezwa Februari 28 dhidi ya Aston Villa.
Sir Alex Ferguson amezungumzia sakata hilo la Ferdinand kwa kusema: “Sisi tuna wasiwasi na hiyo kauli rufaa haina misingi thabiti! Marefa wenye uzoefu mkubwa kwenye Ligi Kuu ni Alan Wiley na Steve Bennett. Wanatakiwa wafuate misingi sawa ya sheria! Kwa Rio, Bennett anasema ni kosa lakini kwa Mascherano Wiley anasema si kosa! Vitendo vya Wachezaji hao wawili ni sawa kabisa! Ukisema rufaa haina misingi kwa jinsi Marefa hao wawili walivyoamua tofauti kwa kosa la aina moja unapingana!”

No comments:

Powered By Blogger