Tuesday 13 April 2010

Chelsea kakamata usukani lakini njia ni Mahandaki matupu!!!
Mbio za kuelekea Ubingwa wa Ligi Kuu na ile vita ndogo ya kuchukua nafasi ya 4 vimepamba moto na kimsimamo Chelsea wako kwenye usukani katika kuwania Ubingwa na Manchester City wanaelekea kuinyakua nafasi ya 4 itakayowafanya wacheze UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Sare ya Manchester United kwa Blackburn na Man City kuibamiza Birmingham ndio vimefungua pazia kuona wazi wazi mwelekeo wa Ligi ulivyo.
Endapo Chelsea leo usiku watawafunga Bolton watakuwa pointi 4 mbele kileleni na labda wapate matokeo mabovu mno kwenye mechi 4 zitakazobakia ndio waukose Ubingwa.
Huku mechi zikizidi kuyoyoma, kauli mbiu kwa Wadau imekuwa ni kuweka presha lakini Man United na Arsenal, hivi karibuni, zimeshindwa kuipa presha Chelsea.
Lakini siku zote hakuna alie na Ubingwa hadi umelitwaa Kombe mkononi na kwa Chelsea inabidi washinde mechi zao ili wawe Mabingwa.
Mara kadhaa Msimu huu, Chelsea wamekuwa wakishika hatamu na mara kadhaa wamekuwa wakiteleza.
Ingawa mechi zinazidi kuyoyoma, nani anasema hilo haliwezi kutokea tena hasa kwa vile wana mechi ngumu za ugenini na Tottenham ikiwa ni dabi ya London na ile ya Anfield na Liverpool?
Hata hivyo, ili wanufaike na kuteleza kwa Chelsea, ni lazima Manchester United na Arsenal washinde mechi zao.
Hilo kwa Man United linamaanisha lazima wakienda kwa Mahasimu wao wakubwa Manchester City, ndani ya Uwanja wa City of Manchester Jumamosi, ushindi ndio kitu pekee wanachotakiwa kukipata.
Wakifungwa mechi hiyo, basi Ubingwa bai bai Msimu huu.
Man United wakishinda mechi hiyo ya Jumamosi, presha itahamia kwa Chelsea wanaocheza baadae siku hiyo na Tottenham kwani wanajua Man United wako nyuma kwa pointi moja tu [hii ikiwa Chelsea ataifunga Bolton leo] na kila mtu anajua ukiwa na presha ni rahisi makosa kufanyika na lolote kutokea.
Lakini, hata kama Man United wataifunga Man City, Ubingwa bado mgumu kwani njia yao pekee ni kwanza kushinda mechi zao zote na pili Chelsea wateleze.
Arsenal nao wako kama Man United- ni lazima washinde mechi zao zote na Chelsea wateleze.
Arsenal wanaanza Jumatano kwa dabi ya Timu za London ya Kaskazini watakapoenda White Hart Lane kucheza na Tottenham ambao nao bado wanalilia nafasi ya 4.
Ni lazima Arsenal ashinde mechi hii na asiposhinda ni balaa.
Na hata wakishinda, mbele wana vigingi vingine navyo ni Man City watakaokwenda Emirates na pia safari ya Arsenal kwenda Ewood Park, Uwanja ambao Chelsea na Man United waliambua droo tu walipocheza na Blackburn.
Mbali ya sakata hilo na mahesabu hayo makali ya Nani Bingwa kati ya Chelsea, Man United na Arsenal, pia utamu upo kwenye kitimtim cha nani atachukua nafasi ya 4 na hivyo kuungana na Chelsea, Man United na Arsenal kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Man City ndio wanaishikilia nafasi hiyo ya 4 na inaelekea wao ndio watainyakua labda wavurunde.
Wengine wanaoiwania nafasi hiyo, na kimahesabu bado wamo kwenye vita hiyo, ni Tottenham, Liverpool na Aston Villa.
Kwa Liverpool na Aston Villa huenda ikawa finyu kuinyakua nafasi hiyo lakini Tottenham bado matumaini makubwa yapo ingawa njia yao ni ngumu kwani inabidi wacheze na Arsenal, Chelsea na Man United.
Ni mahesabu makali lakini bora tukae na kusubiri nini kitatokea kuanzia sasa hadi Mei 9 Ligi itakapofika tamati.
Berbatov nje?
Wadau wengi wanadai Dimitar Berbatov hajafanya lolote Manchester United tangu atue hapo Septemba 2008 kwa dau la Pauni Milioni 31 kutoka Tottenham na kuna tetesi za Magazetini kuwa mwishoni mwa Msimu atatemwa.
Ukweli ni kuwa tangu aanze kuchezea Man United, Berbatov amekuwa chaguo la pili katika mechi zote kubwa na pale alipokuwa chaguo la kwanza, ameshindwa kuwika na amekuwa akiwakera Washabiki wengi.
Inadaiwa Sir Alex Ferguson ameshachoshwa na atamuuza ili kuwanunua David Silva kutoka Valencia na Karim Benzema wa Real Madrid.
Hata hivyo, Wachunguzi wanaamini Berbatov hatauzwa kwa sababu Man United hawako tayari kumpoteza Straika mwingine baada ya kuwapoteza Cristiano Ronaldo na Carlos Tevez kwa mpigo na pia hata wakiamua kumuuza Berbatoz dau lake litakuwa chini mno na hiyo ni hasara kwa Klabu.

No comments:

Powered By Blogger