Thursday 15 April 2010

Ze Gunners yabondwa, Chelsea njia nyeupeeee…….!!!
Jana, Uwanjani White Hart Lane, Tottenham waliibonda Arsena kwa bao 2-1 katika dabi ya Ligi Kuu England ambayo huenda ndio imemaliza kabisa ile kiu ya Arsenal ya angalau kupata Kikombe kimoja Msimu huu na kuumaliza ule ukame wao wa kutokuwa na Kikombe tangu 2005 kwani sasa wako nyuma ya vinara Chelsea kwa pointi 6, nyuma ya Man United kwa pointi 2 na mechi zimebaki 4 tu.
Ushindi huu kwa Tottenham bado unaweka hai matumaini yao ya kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya 4 na hivyo kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao kwani sasa wako nafasi ya 5 pointi moja tu nyuma ya Manchester City walio nafasi ya 4 huku Timu hizo mbili zikiwa zimebakiza mechi 5 kila mmoja.
------------------------------------------------
MSIMAMO LIGI KUU [Kwa Timu za juu]:
1. Chelsea mechi 34 pointi 77
2. Man United mechi 34 pointi 73
3. Arsenal mechi 34 pointi 71
4. Man City mechi 33 pointi 62
5. Tottenham mechi 33 pointi 61
6. Liverpool mechi 34 pointi 56
7. Aston Villa mechi 33 pointi 55
8. Everton mechi 34 pointi 51
9. Birmingham mechi 34 pointi 46
10.Stoke mechi 33 pointi 43
11.Blackburn mechi 34 pointi43
-----------------------------------------------
Alikuwa ni Mchezaji aliekuwa akicheza Ligi kwa mara ya kwanza, Danny Rose, aliipeleka Tottenham mbele kwa mzinga wa mita 30 kwenye dakika ya 10.
Dakika moja baada ya haftaimu, Gareth Barry akaipatia Spurs bao la pia alipopokea pasi toka kwa Jermain Defoe.
Kipa wa Spurs, Heurelho Gomes aliokoa michomo mitatu ya Arsenal lakini baadae akashindwa kumzuia Niklas Bendtner wa Arsenal kuifungia Timu yake bao.
Huu ulikuwa ushindi wa kwanza wa Tottenham kwa Arsenal katika Ligi tangu Novemba 1999 na mechi 20 zimepita kati yao tangu wakati huo.
Wote, Tottenham na Arsenal, waliingia kwenye dabi ya jana wakitoka kwenye vipigo vitakatifu pale Tottenham alipobwagwa nje ya FA Cup na Timu hoi bin taabani Portsmouth walipochapwa 2-0 kwenye Nusu Fainali Uwanjani Wembley Jumapili na Arsenal kupata kipigo cha mbwa kachoka huko Nou Camp cha bao 4-1 toka kwa mtu mmoja tu, Lionel Messi, kilichowafanya Barcelona waisokomeze Arsenal nje ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Arsenal, kwa mara nyingine tena, walipata pigo pale Beki wao Thomas Vermaelen aliposhindwa kuendelea na mechi na kutoka nje akichechemea na nafasi yake kuchukuliwa na Mkongwe Mikael Silvestre alieungana na Mkongwe mwingine Sol Campbell kama Masentahafu.
Lakini Arsenal walipata faraja kidogo walipomwona Straika wao Robin van Persie akiingizwa na kucheza baada ya miezi mitano nje akiuguza enka na kuingia kwake kulimfanya Kipa wa Spurs Gomes aokoe mipira miwili hatari toka kwake.
Aston Villa 2 Everton 2
Bao la kujifunga mwenyewe la Phil Jagielka katika dakika za majeruhi zimewapa sare Aston Villa wakiwa nyumbani Villa Park walipocheza na Everton kwenye Ligi Kuu hapo jana.
Tim Cahill wa Everton ndie aliepachika bao la kwanza kwa Everton kufuatia krosi ya Leighton Baines na kichwa cha Gabriel Agbonlahor kiliwasazishia Villa lakini haikuchukua muda mrefu Tim Cahill akafunga bao la pili kwa Everton.
Sare hii si matokeo mazuri kwa Timu zote hizo mbili, Villa wakipoteza matumaini ya kupata nafasi ya 4 na Everton sasa wanabanwa kuipata nafasi ya kucheza EUROPA LIGI.
Wigan 0 Portsmouth 0
Kwenye mechi ya Ligi Kuu hapo jana, Wigan jana ilishindwa kuifunga Timu hoi bin taabani Portsmouth ambayo tayari ishashushwa Daraja na jana iliingia Uwanjani ikiwa Timu ya kuungwaungwa tu huku Meneja wao Avram Grant akishindwa kukamilisha idadi ya Wachezaji wa Akiba wanaoruhusiwa kuwa benchi ya Wachezaji 7 pale alipolazimika kuwa na Wachezaji wanne tu benchi kutokana na matatizo ndani ya Klabu hiyo.
Portsmouth walibadilisha Wachezaji wanane toka Kikosi kilichoifunga Tottenham 2-0 Jumapili na kuwafikisha Fainali za Kombe la FA lakini Wigan walishindwa kuwafunga.
Sare hii imewafanya Wigan wawe pointi 5 juu ya zile Timu 3 za mwisho ambazo zipo eneo hatari la kushushwa Daraja.

No comments:

Powered By Blogger