Monday 12 April 2010

Pompey kukata rufaa ili wacheze Ulaya
Portsmouth watakata rufaa kwa FA ili waruhusiwe kupata leseni ya UEFA itakayowafanya waweze kecheza michuano ya Ulaya ya EUROPA LIGI Msimu ujao.
Kwa kuingia Fainali ya Kombe la FA, Portsmouth ambao wameshushwa Daraja, wamefuzu kucheza mechi za EUROPA LIGI kwa vile Chelsea, watakaocheza nao Fainali ya Kombe la FA, moja kwa moja watacheza UEFA CHAMPIONS LIGI kwa kumaliza Ligi Kuu nafasi 3 za juu.
Lakini kwa sababu Portsmouth iko chini ya Msimamizi Maalum alieteuliwa ili kuinusuru Klabu hiyo isifilisiwe, hairuhusiwi kuomba leseni ya UEFA.
Msimamizi Maalum, Andrew Andronikou, ametamka kuwa wataka rufaa kupinga hatua hiyo ingawa alikiri wao walishindwa kuomba leseni kabla ya siku ya mwisho ya maombi, tarehe yake ilikuwa Machi 1, kwa sababu Klabu ilikuwa taabani kifedha.
Burnley yamfungia Mchezaji wake
Kiungo wa Burnley Joey Gudjonsson amefungiwa wiki mbili kwa matamshi yake kuhusu Meneja wa Klabu hiyo Brian Laws na ametakiwa asikanyage Klabuni hadi uchunguzi ukamilike.
Inadaiwa Mchezaji huyo alisema kuwa Brian Laws ameshindwa kuikontroli Timu na Wachezaji wote wamekosa imani kwake na ndio maana Timu inafungwa ovyo.
Kauli hiyo inadaiwa kutolewa kabla Burnley haijakung’utwa 6-1 na Manchester City kwenye Ligi Kuu.
Jumamosi, Burnley iliipiga Hull City bao 4-0.
Coyle amcheka Fergie kwa kusema Bolton ubwete kwa Chelsea
Owen Coyle amepuuza kauli ya Sir Alex Ferguson kwamba pambano la Chelsea na Bolton hapo kesho huko Stamford Bridge ni mechi rahisi kwa Chelsea.
Ikiwa Chelsea watashinda hiyo kesho watakuwa pointi 4 mbele ya Manchester United ambao jana walitoka 0-0 na Blackburn.
Owen Coyle, Meneja wa Bolton, amesema wao wana kila sababu ya kuitilia ngumu Chelsea hasa kwa vile wako pointi 5 juu ya zile Timu 3 za mwisho zilizo eneo la kushushwa Daraja.
Coyle amesema: “Ni uamuzi wake kusema lolote! Sisi tutakazania nini cha kufanya na si nini kimesemwa.”
Wakati huo huo, Nahodha wa Bolton, Kevin Davies, amesema anadhani Mastraika wa Chelsea, Didier Drogba na Nicolas Anelka, hawana uhusiano mzuri na hilo huenda litaathiri Timu hiyo.
Liverpool kupigwa bei
Wamarekani, Tom Hicks na George Gillett, wanaoimiliki Liverpool wanategemewa kuiingiza Klabu hiyo sokoni wiki hii kufuatia hatua yao ya kuiteua Benki ya Barclays kusimamia zoezi hilo na pia kumteau Martin Broughton, aliewahi kuwa Mwenyekiti wa British Airways, kuwa Mwenyekiti wa Liverpool mwenye jukumu la kusaka Wawekezaji.
Wakiwa wanakabiliwa na deni kubwa, Wamarekani hao wamekubaliana na Wadai wao kusogeza mbele ulipaji wa deni hilo ili waendelee kutafuta Wanunuzi au Wawekezaji.
Wamarekani hao, ambao wanapingwa vikali na Mashabiki wa Klabu hiyo, wanataka kitita cha Pauni Milioni 500 ili kuiuza Liverpool.

No comments:

Powered By Blogger