Sunday 11 April 2010

POMPEY…..Jana wameshushwa Daraja, Leo watinga Fainali FA CUP!!!
Hii ndio hadithi ya Sinderela ama ile stori ya kulala Maskini, kuamka Tajiri!!!
Portsmouth imepita kwenye Msimu wa balaa kabisa na nusura Klabu ife pale iliponusurika kufilisiwa lakini haikunusurika kushuka Daraja hasa ilipokatwa pointi 9 na jana ushindi wa West Ham ndio ukawahakikishia kucheza Ligi ya Coca Cola Championship Msimu ujao.
Lakini leo, ikiwa Uwanjani Wembley kwenye Nusu Fainali ya FA Cup, ilimudu kuibwaga Tottenham kwa bao 2-0 na kutinga Fainali hapo Mei 15 itakapocheza na Chelsea ambao jana waliwatoa Aston Villa bao 3-0.
Hadi dakika 90 ngoma ilikuwa 0-0 na ndipo ikaja ile nusu saa ya nyongeza na ndipo nyota ya Pompey ikaanza kuchomoza katika mechi ambayo muda wote walikuwa ni Timu ya pili kwa ubora.
Kwenye dakika ya 99 Pompey walipata frikiki iliyodondoshwa ndani ya boksi lakini katika harakati za kuokoa Beki wa Tottenham Dawson akateleza na Straika wa Pompey Frederic Piquionne akawa mwepesi na kuwahi hiyo ‘luzi boli’ na kuipenyeza kumpita Kipa Gomes.
Hadi nusu ya kwanza ya dakika 30 za nyongeza kwisha, Pompey walikuwa mbele kwa bao 1-0 lakini Spurs walikuwa wakishambulia mfululizo.
Huku Spurs wakiendelea kushambulia na Pompey kulinda bao lao ikafika dakika ya 117 na shambulio la Spurs likaokolewa na Pompey na wakaanza kufanya ‘kaunta ataki’ ya haraka kupitia Aruna Dindane ambae aliwahadaa Mabeki waliodhani atatoa pasi lakini akachanja mbuga mwenyewe kuingia ndani ya boksi na akaangushwa na Wilson Palacios.
Refa Alan Wiley akaashiria penalti na Kevin-Prince Boateng akafunga penalti hiyo.
AMINI USIAMINI….POMPEY 2 SPURS 0….NA WAKO FAINALI!!!!!!!!
Vikosi vilivyoanza:
Tottenham: Gomes, Corluka, Dawson, Bassong, Bale, Bentley, Huddlestone, Palacios, Modric, Crouch, Defoe.
Akiba: Alnwick, Pavlyuchenko, Gudjohnsen, Kranjcar, Rose, Livermore, Assou-Ekotto.
Portsmouth: James, Finnan, Rocha, Mokoena, Mullins, Brown, Wilson, Yebda, Dindane, Piquionne, Boateng.
Akiba: Ashdown, Diop, Utaka, Smith, Hughes, Kanu, Basinas.
Refa: Alan Wiley

No comments:

Powered By Blogger