Sunday 19 September 2010

Berbatov Shujaa Old Trafford!!!
• Apiga Hetitriki!!!!!
• Man United 3 Liverpool 2
SHUJAA BERBATOV
Dimitar Berbatov amekuwa akiandamwa na wengi tangu atue Old Trafford akitokea Tottenham Hotspurs kwa uchezaji wake wa kupooza na kuua mipira ya kasi, ingawa siku zote Meneja wake Sir Alex Ferguson amekuwa akisistiza huyo ni kipaji cha hali ya juu, na leo kwenye BIGI MECHI ya Uingereza kati ya Mahasimu wa karne na karne, Manchester United na Liverpool, Berbatov amethibitisha yeye ni kiboko pale alipowapa raha Mashetani Wekundu kwa kupachika bao zote 3 huku bao zote zikiwa ni tamu na za ufundi wa hali ya juu.
Hii ni mechi ambayo Manchester United waliitawala na walistahili ushindi lakini nusura waimwage kama walivyofanya kwenye mechi zao mbili za Ligi Kuu zilizopita walipotoka sare na Fulham na Everton kwani leo waliongoza 2-0 na kuwaruhusu Liverpool kurudisha na kufanya mechi iwe 2-2 lakini leo Shujaa ni Berbatov ambae alifunga bao lake la 3 na la ushindi kwa Man United.
Berbatov alifunga bao la kwanza dakika ya 42 kwa kichwa kufuatia kona ya Ryan Giggs na hadi mapumziko Man United 1 Liverpool 0.
Ndipo kwenye dakika ya 52 pande refu la Darren Fletcher kumlenga Nani kwenye winga ya kulia na krosi ya Nani golini ilimkuta Berbatov kwenye boksi huku akiwa amelipa mgongo goli, akaukontroli mpira kwa paja la mguu mmoja na kuachia tiktaka iliyogonga posti ya juu na kujikita wavuni.
Hakika hilo ni miongoni mwa Magoli ya Msimu kama si Goli la Msimu.
Lakini Liverpool wakafufuka na ndani ya dakika 6, wakafunga bao la kwanza kwa penalti baada ya Torres kuangushwa na Johny Evans na la pili kwa frikiki, zote zikipigwa na Nahodha wao Steven Gerrard.
Hizo zilikuwa ni dakika ya 64 na 70.
Lakini Shujaa ni Dimitar Berbatov.
Zikiwa zimebaki dakika 6 mechi kwisha, krosi ya John O’Shea iliunganishwa kwa kichwa na Berbatov na kuwainua Manchester United kwa furaha.
Vikosi vilivyoanza:
Man United: Van der Sar, O'Shea, Vidic, Jonny Evans, Evra, Nani, Fletcher, Scholes, Giggs, Berbatov, Rooney.
Akiba: Kuszczak, Brown, Owen, Anderson, Smalling, Macheda, Gibson.
Liverpool: Reina, Johnson, Carragher, Skrtel, Konchesky, Meireles, Poulsen, Maxi, Gerrard, Cole, Torres.
Akiba: Jones, Agger, Jovanovic, Kyrgiakos, Babel, Lucas, Ngog.
Refa: Howard Webb

No comments:

Powered By Blogger