LIGI KUU ENGLAND: RATIBA:
[Saa za Bongo]
Jumamosi, 25 Septemba 2010
[saa 8 dak 45 mchana]
Man City v Chelsea
[saa 11 jioni]
Arsenal v West Brom
Birmingham v Wigan
Blackpool v Blackburn
Fulham v Everton
Liverpool v Sunderland
West Ham v Tottenham
Jumapili, 26 Septemba 2010
[saa 8 mchana]
Bolton v Man Utd
[saa 10 dak 5 jioni]
Wolverhampton v Aston Villa
[saa 12 dak 10]
Newcastle v Stoke
TATHMINI:
Man City v Chelsea
Vinara wa Ligi Kuu ambao pia ni Mabingwa Watetezi Chelsea wanasafiri hadi Uwanja wa City of Manchester kuikwaa ‘Timu Tajiri’ Manchester City, pambano ambalo wengi wanahisi huu ndio mtihani wa kwanza mgumu wa Chelsea baada ya kuanza na Timu ubwete kwenye Ligi Msimu huu.
Timu zote hizi mbili zilifungwa na kutupwa nje ya Carling Cup katika mechi zilizochezwa majuzi huku Chelsea wakibwagwa 4-3 na Newcastle na Man City kuchapwa 2-1 na West Bromwich.
Liverpool v Sunderland
Hii imekuwa Wiki ngumu kwa Liverpool kwani Jumapili iliyopita walichapwa 3-2 na Mahasimu wao Manchester United kwenye mechi ya Ligi Kuu na juzi wakatolewa nje ya Carling Cup na Timu ndogo ya Daraja la Ligi 2, Northampton, iliyowashinda kwa penati 4-2 baada ya mechi kwisha 2-2.
Sunderland, wiki iliyopita, walitoka sare 1-1 na Arsenal.
Arsenal v West Brom
Wakiwa kwao Uwanja wa Emirates, Arsenal wanaikaribisha West Brom Timu ambayo imepanda Daraja Msimu huu na inayojikongoja vizuri tu.
Wiki iliyopita Arsenal walipokwa tonge mdomoni pale Sunderland waliposawazisha dakika za majeruhi na kumfanya Bosi wao Arsene Wenger kuwaka na hatimaye kupigwa Faini na FA na kufungiwa mechi moja baada ya kumvaa Refa wa Akiba akilalamikia muda.
Wenger ameshatumikia adhabu yake ya mechi moja hapo juzi kwenye mechi ya Carling Cup walipoipiga Tottenham 4-1 baada ya muda wa nyongeza.
Mara ya mwisho kwa West Bromwich kutua Jijini London Msimu huu ilikuwa ni huko Stamford Bridge ambako walichapwa 6-0 na Timu yake ya zamani ya Bosi wao Robert Di Matteo, Chelsea.
West Ham v Tottenham
Hii ni dabi ya Timu za London Uwanjani Upton Park na West Ham, chini ya Meneja Avram Grant, bado wanasuasua kwenye Ligi Kuu wakiwa mkiani na wana pointi 1 tu baada ya mechi 5.
Tottenham wapo nafasi ya 5 wakiwa na pointi 8.
Fulham v Everton
Jumanne iliyopita, Everton walitolewa nje ya Carling Cup na Timu ya chini Brentford na kwenye Ligi Kuu Msimu huu, hawajashinda hata mechi moja na mechi hii itakayochezwa Craven Cottage, nyumbani kwa Fulham, ni ngumu kwao.
Msimu huu, katika mechi zao 5 za Ligi Kuu, Fulham hawajafungwa baada ya kushinda moja na kutoka sare 4 lakini kesho watakuwa na ubutu mbele baada ya Mafowadi wao wawili wa kutumainiwa, Moussa Dembele na Bobby Zamora, kuwa majeruhi.
Blackpool v Blackburn
Hii ni mechi ya pili ya nyumbani kwa Blackpool waliopanda Daraja Msimu huu na ambao wako nafasi ya 9 wakiwa na pointi 7 huku Blackburn wakiwa nafasi ya 14 wakiwa na pointi 5.
Birmingham v Wigan Athletic
Wigan, ambao wameonyesha udhaifu mkubwa kwenye difensi, wapo nafasi ya 18 wakiwa na pointi 4 na watakuwa wageni wa Birmigham ambao hawafungiki wakiwa nyumbani Uwanja wa Mtakatifu Andrew.
Bolton v Man United
Kawaida Manchester United hupata wakati mgumu wakiwa Uwanja wa Reebok, nyumbani kwa Bolton, lakini safari hii ndio kwanza wametoka kuwabonda Mahasimu wao Liverpool kwa bao 3-2 Jumapili iliyopita na Jumatano, Kikosi chao cha pili, kiliichapa Scunthorpe 5-2 kwenye Carling Cup.
Hivyo, Manchester United watakaza uzi ili washinde kabla hawajasafiri kwenda Spain kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI na Valencia siku ya Jumatano Septemba 29.
Wolves v Aston Villa
Hii ni dabi ya Timu za Katikati ya England, eneo la Midlands, na mechi ya kwanza kwa Meneja mpya wa Aston Villa, Gerard Houllier, ambae siku za nyuma alikuwa Liverpool.
Newcastle v Stoke City
Newcastle wapo nyumbani Uwanja wa St James Park na bado wana furaha ya kuichapa Chelsea 4-3 huko Stamford Bridge na kuitupa nje ya Carling Cup hivi juzi.
Newcastle wapo nafasi ya 6 kwenye Ligi na Stoke wapo nafasi ya 17.
Hargreaves aanza mazoezi na Man United
Owen Hargreaves, Miaka 29, ameanza tena mazoezi na Kikosi cha kwanza cha Manchester United baada ya kutoka matibabu huko Marekani ambako alifanyiwa operesheni ya magoti yake yote mawili Miaka miwili iliyopita lakini ikabidi Mwezi Julai arudishwe tena kwa Madaktari baada ya kusikia maumivu tena.
Meneja wa Man United, Sir Alex Ferguson, amethibitisha kurudi kwa Hargreaves na amesema: “Ameanza mazoezi na Kikosi cha Kwanza na alionekana safi sana. Hii ni silaha mpya kwangu.”
No comments:
Post a Comment