Sunday 19 September 2010

Wenger awaka, pengine kupigwa Rungu na FA!!
Arsene Wenger alilipuka mara baada ya Darren Bent kusawazisha bao kwenye dakika za majeruhi na kuifanya mechi ya Ligi Kuu hapo jana kati ya Sunderland na Arsenal kwisha 1-1.
Goli la Bent liliingia kwenye dakika ya 95 baada ya bango la muda wa nyongeza kuonyeshwa dakika 4 na Wenger amedai: “Ukiwa na saa unaikontroli! Ni kitu rahisi.”
Wenger alionekana akimvaa Refa wa Akiba Martin Atkinson mara baada ya Bent kufunga goli hilo na huenda hilo likamtia matatani na FA.
Lakini, Wenger baadae alikana kumsakama Atkinson na kusema: “Sikulalamika kwa Mtu. Katika zile dakika 4 za nyongeza kulikuwa hamna kitu cha kufanya muda uongezwe zaidi ya hapo. Lakini najua Refa anaweza kuongeza muda zaidi ya dakika 4.”
Katika mechi ya jana, Arsenal walipata bao la bahati baada ya shuti la kuosha mbele la Anton Ferdinand kuzuiwa na Cesc Fabregas na mpira kurudi golini na kutinga.
Arsenal wangeweza kufunga bao la pili lakini penalti iliyopigwa na Tomas Rosicky ilipaa juu na hilo lilimkera Wenger ambae alitamka: “Sikudhani kama Rosicky angepiga, nilijua ni Samir Nasri.”
Vile vile, Wenger alilalamika kuhusu kupewa Kadi Nyekundu Mchezaji wake Song na amedai Kadi ya Njano ya kwanza aliyopewa ilikuwa kali mno na ya Pili ilikuwa pia haistahili.

No comments:

Powered By Blogger